Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Hassan Rugwa amewataka watumishi wa Umma katika Halmashauri ya Mji Kasulu kushirikiana na kufanya kazi kwa weledi ili kuyafikia malengo yaliyowekwa na Serikali kiutendaji kazi katika utumishi wa Umma.
Rugwa ametoa kauli hiyo alipozungumza na watumishi hao katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Maendeleo sambamba na kusikiliza kisha kutatua kero za watumishi wa Umma katika Halmashauri nane (8) za Mkoa wa Kigoma.
‘’Sio kila wakati inahitajika rasilimali fedha ili kutimiza malengo tuliyojiwekea bali kufanya kazi huku tukidumisha udugu hii inaleta fahari na kudumisha mahusiano mema katika utumishi wetu wa Umma na kuleta matokeo chanya’’ alisisitiza Rugwa.
Katika kuhakikisha ufanisi kwenye utendaji kazi katika Halmashauri hiyo, Rugwa amemuagiza Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo kufuatilia ili kubaini wakuu wa Idara na Vitengo wanaokaimu kwa muda mrefu huku wakiwa na sifa waweze kuthibitishwa na kuwa wakuu kamili wa Idara hizo.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo amewakumbusha watumishi kuzingatia utaratibu wa kufanya manunuzi kwa kutumia mfumo mpya wa Nest na kuachana na mifumo ya zamani kwani ni kosa kisheria.
''Hakikisheni manunuzi yote yanafanyika kwa kuzingatia mfumo huu mpya kwani ni maelekezo ya Seerikali, kumbukeni kukiuka maelekezo hayo zipo adhabu za kisheria zilizowekwa hivyo tutumie wataalam wenye weledi wa matumizi ya mfumo ili kutujengea uwezo ili kila mtu aweze kufanya manunuzi ya kiofisi kwa ufasaha'' alisema Rugwa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa