Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amewaelekeza wakurugenzi watendaji wa Halmashauri nane za Mkoa wa Kigoma kuhuisha zoezi la kupima na kuandaa hati miliki kwa ajili ya maeneo yote yanayomilikiwa na Serikali mkoani Kigoma.
Rugwa ametoa maelekezo hayo akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa utekelezaji miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Kasulu na kusisitiza kuwa utekelezaji wa agizo hilo utapunguza uwepo wa migogoro ya Ardhi baina ya Serikali na wananchi wanaovamia maeneo yanayomilikiwa na Taasisi za Umma.
Amesema ukosefu wa hati miliki katika maeneo ya Taasisi za Umma imekuwa ni changamoto ya mudamrefu katika halmashauri na kusababisha upotevu mkubwa wa Fedha na muda kutokana na ufuatiliaji wa mashauri hayo katika ngazi mbalimbali za kimahakama.
‘’Nitumie nafasi hii kutoa maelekezo haya kwa wakurugenzi ili waweze kuwaelekeza na kuwasimamia viongozi wote wa Taasisi za Umma kushirikiana na wataalam wa Ardhi kwa lengo ya kuyatambua maeneo tengefu au yale yenye miundombinu kisha kuyaandalia utaratibu wa kuyawekea hati miliki hizo’’ amesisitiza Rugwa.
Amesema serikali inawekeza kiasi kikubwa cha fedha katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Umma hivyo kukosekana kwa hati katika maeneo hayo ni sawa na kushindwa kuheshimu juhudi za serikali katika kutoa huduma na kuyaweka katika hatari ya kuvamiwa na kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Aidha Rugwa amesisitiza kuwa halamshauri zote zinatakiwa kuanza kutekeleza agizo hilo kuanzia Julai Mosi, 2024 ambapo katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia tarehe hiyo, kila taasisi za Umma katika halmashauri hizo itatakiwa kuwa imekamilisha zoezi hilo.
Albert Mhoza mkazi wa Kijij cha Chekenya wilayani Kasulu amesema iwapo serikali itatekeleza zoezi hilo la kuyapima na kuyawekea hati miliki maeneo hayo, itapunguza migogoro ya ardhi na wananchi kwani tabia ya uvamizi hutokana na maeneo mengi kukosa utambulisho wa umiliki wa serikali pamoja na kutoendelezwa kwa muda mrefu.
‘’Maeneo ya Taasisi za kielimu na Afya zimekuwa zikiongoza kwa watu kuvamia maeneo hayo na kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo uharibifu wa hifadhi za mazingira ikiwa ni pamoja na ukataji wa miti na uharibifu wa miundombinu inayotumika kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii’’ amesisitiza.
Aidha kupitia ziara hiyo Katibu Tawala amewasisitiza watendaji katika halmashauri ya Kasulu kuongeza kasi katika kusimamia miradi ya Maendeleo ili iweze kukamilika kwa wakati na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Kiongozi huyo ametembelea na kukagua ukamilishwaji wa jengo la upasuaji katika Hoapitali ya Wilaya ya Kasulu, jengo la Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na ujenzi wa Zahanati ya Chekenya.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa