Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amempongeza Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi sahihi ya kutoa Fedha zaidi ya Shilingi Bil. 7.61 kwa ajili ya Ujenzi wa Vyumba 358 vya Madarasa kwa Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajia kuanza kidato cha kwanza Mwaka 2023.
Fedha hizo zilizotolewa na Mhe. Rais, zimelenga kumpunguzia mzigo wa michango mwananchi wa kawaida na kuhakikisha kila Mwanafunzi aliyefaulu Elimu ya Msingi, anajiunga na kuendelea ngazi ya Sekondari bila kuwepo kwa changamoto hiyo ambayo hapo awali imechangia kiasi kikubwa katika kuathiri na kushusha ufanisi katika Taaluma.
Andengenye ametoa pongezi hizo huku akisisitiza wanaofanya kazi za ujenzi wa madarasa hayo watangulize uzalendo kwa kuhakikisha kazi wanazozifanya zinaakisi Thamani halisi ya Fedha zilizotolewa na Mhe. Rais
‘‘Ili tuonyeshe ni kwa kiasi gani sote tunathamini maamuzi ya Rais wetu, tutangulize uzalendo kwa kuwa waadilifu katika matumizi ya fedha hizo pamoja na kuhakikisha kazi zinazofanyika zinalingana na Thamani ya fedha zilizotolewa’’
‘‘Hapa tunajenga chetu kwa manufaa yetu na kizazi chetu, hivyo hakuna haja ya kufanya udanganyifu wa aina yoyote na atakayefanya hivyo ajue analikosea Taifa na kujikosesha haki yake ya msingi yeye na vizazi vijavyo’’ amesema Andengenye.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewapongeza wanawake wanaotumia fursa za utekelezwaji miradi mbalimbali ya Maendeleo katika maeneo yao kwa lengo la kujipatia ajira za muda mfupi ili kujiongezea kipato na kumudu majukumu mbalimbali ya kimaisha.
Amesema wanawake hao wawe mfano wa kuigwa kwa wenzao katika Mkoa wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla, kwa kuchangamkia fursa zinazojitokeza ili kujipatia kipato halali kupitia shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo zinazotekelezwa na Serikali katika Maeneo yao.
Bi. Adelina Leonard, amesema utekelezaji wa miradi ya Serikali unawanufaisha kwa kupata ajira za muda ambazo zinawapatia kipato kwa ajili ya kujikimu kimaisha.
‘‘Kupitia miradi hii tunapata kazi ambazo zinatuweaesha kupata fedha za kununua mahitaji muhimu ya familia, lakini pia tunaposhirikiana na mafundi wazoefu nasisi tunapata ujuzi wa kiufundi ambapo tutaweza kwenda kufanya kazi sehemu nyingine mara mradi huu utakapokamilika’’ amesema Bi. Adelina.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa