Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameuelekeza Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu kutambua na kuyapatia Hati Miliki Maeneo yote yanayomilikiwa na Halmashauri hiyo ili kuepuka Migogoro ya mara kwa mara dhidi ya wananchi kuhusiana na Umiliki wa Ardhi.
Kiongozi huyo ametoa Melekezo hayo leo Juni 13, 2023 alipozungumza katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu uliolenga kujadili Hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2021/2022.
Amesema Mojawapo ya Jukumu la Menejimenti katika Halmashauri ni kufuatilia kwa ukaribu na kuhakikisha Mali zote za Serikali zilizo chini ya Halmashauri husika zinabainishwa kisha kufanyiwa mchakato umiliki kisheria.
Ameendelea kufafanua kuwa, Migogoro ya Ardhi imeendelea kuzitia hasara Halmashauri nyingi mkoani Kigoma kutokana na uwepo wa kesi za muda mrefu, jambo linaloweza kutatuliwa kwa kuweka alama katika maeneo yote yanayomilikiwa na Halmashauri hizo hali itakayosaidia kuondoa uwezekano wa wananchi kuyavamia na kujimilikisha kinyume cha Sheria.
‘‘Taratibu za umiliki wa Ardhi zitakapokamilishwa kisheria, hakikisheni mnaanzisha Daftari maalum ambalo litatumika kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu za maeneo hayo pamoja na Mali nyingine za Halmashauri kwa lengo la kurahisisha utambuzi wa mali hizo na ufuatiliaji wake’’ amesema Andengenye.
Kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali imeonesha Halmashauri hiyo imefanikiwa kupata Hati Safi ya Ukaguzi wa Hesabu za Seriali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa