Watendaji wa Serikali katika Halmashauri za Mkoa wa Kigoma wametakiwa kuongeza kasi katika kusimamia na kukusanya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa lengo la kuwaletea Maendeleo Wananchi.
Akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema kiwango cha Ukusanyaji wa mapato kitaongezeka kwa kutatua changamoto za uibuaji na usimamizi mzuri wa vyanzo vipya vya Mapato.
‘’Nijukumu letu viongozi wa Serikali katika Halmashauri zetu kuhakikisha utaratibu wa kukusanya Mapato ya ndani unazingatiwa kwa kufuata miongozo pamoja na kudhibiti viashairia vya upotevu wa makusanyo hayo’’ amesema.
Amewaeleza wajumbe kuwa, Halmashauri zinamapato ya kutosha lakini changamoto kubwa ni usimamizi wa vyanzo hivyo, wakusanya mapato pamoja na kutokufuatilia na kubaini ufanisi wa vitendea kazi.
Akiwasilisha taarifa ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, Katibu Tawala Mkoa Kigoma Albert Msovela amesema Mkoa ulipokea kiasi cha Shilingi 197,461,488,206 kwa ajili ya kutekeleza Bajeti ya Maendeleo.
Amesema kutokana na fedha hizo, mkoa umefanikiwa kutekeleza Miradi ya Ujenzi wa Nyumba, Ofisi za wakuu wa wilaya, kukarabati majengo mbalimbali ya Ofisi ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo shughuli hizo zimegharimu Shilingi Bil 2.5.
Msovela amevitaja vipaumbele vya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kuwa ni uimarishaji wa Huduma za Jamii kwa Umma, kuendelea na ujenzi wa nyumba na Ofisi za watendaji wa Serikali, kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kufuatiliaji na kusimamia Shughuli katika Sekta za Elimu, Uchumi na Uzalishaji.
Aidha Msovela amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa Chama cha Mapinduzi kwa ufuatiliaji wao wa karibu katika Miradi mbalimbali inayotekelezwa na kutoa ushauri pale walipoona inafaa kufanya hivyo.
Pia Katibu Tawala amewashukuru watumishi wote wa Serikali kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya mkoani Kigoma katika kuhakikisha wanaihudumia Jamii pamoja na kusimamia vizuri miradi inayotekelezwa na Serikali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa