Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amemuelekeza Waziri wa Nishati kufuatilia na kushughulikia changamoto ya kukatika kwa Umeme mara kwa mara wilayani Kasulu na kuitafutia ufumbuzi wa haraka ili uhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa uhakika na kuruhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Maelekezo hayo ameyatoa alipozungumza na wakazi wa wilaya ya Kasulu akiwa katika ziara yake ya Siku tatu mkoani hapa akiambatana na wajumbe wa Sekretariet ya CCM Taifa kwa lengo la kuhuisha uhai wa chama, kusikiliza na kutatua kero za wananchi amoja na kuhamasisha wakazi kushiriki uchaguzi na kuchagua viongozi bora wakati wa zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa.
Amesema Rais Dkt. Samia amedhamiria kuufungua mkoa wa Kigoma na tayari ameshatoa zaidi ya Shilingi Tril.11 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimba ya Maendeleo ili kuufanya mkoa kuwa Ukanda wa kibiashara na uwekezaji.
‘’Kuna hatua kubwa za kimaendeleo za kujivunia mkoani hapa ikiwemo ujenzi wa barabara za kuunganisha mkoa na mikoa jirani kwa kiwango cha lami, upanuzi wa uwanja wa ndege, ukarabati wa Meli, miradi ya Maji, Elimu pamoja na mkoa kuunganishwa na Gridi ya Taifa, hizi zote ni kazi nzuri zilizofanywa na CCM’’ amesisitiza Nchimbi.
Akitolea ufafanuzi kuhusu changamoto iliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Kasulu mjini Prof. Joyce Ndalichako ya kutokamilika kwa miundombinu katika kituo cha Afya cha Mwami Ntare kilichopo wilayani humo, Dkt. Nchimbi amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI kufuatilia na kuwaagiza watendaji walio chini yake kutoa kiasi cha Shilingi Mil.200 kwa ajili ya kukamilisha kituo hicho na kuruhusu utoaji wa huduma.
Aidha amemuelekeza waziri wa Wizara hiyo kufuatilia na kuhakikisha unapatikana ufumbuzi kuhusu changamoto inayosababisha Kata ya Kagerankanda kutokuwa na diwani ili upatikane ufumbuzi na kata hiyo iweze kuwa na uongozi wake
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255738192977
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa