Kuanzishwa kwa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Mkoani Kigoma kumeelezwa kuwa kutasogeza na kuongeza fursa za utolewaji wa huduma bobezi kutoka kwa Madaktari bingwa pamoja na kuongeza Ikama ya watumishi katika Sekta ya Afya mkoani Kigoma.
Akizungumza kwenye kikao cha kupokea Taarifa ya Maendeleo ya Utekelezaji Mradi wa Ujenzi wa Kampasi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema pamoja na mradi kujielekeza katika kupunguza changamoto za kimatibabu, utaongeza mnyororo wa Thamani na kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Kigoma.
Amesema faida zitakazosababishwa na uwepo wa Kampasi hiyo hazitokuwa upande wa Afya na Elimu pakee bali, kutakuwepo na fursa kwa wafanyabiashara wakubwa na wale wenye mitaji midogo kutoka ndani na nje ya Mkoa pamoja na nchi kuwekeza na kufanya Biashara zao mkoani hapa.
‘’Uwepo wa ongezeko la watu utakaosababishwa na ujio wa Chuo hicho utapanua na kuimarisha Masoko yetu ya bidhaa zinazozalishwa na kupatikana ndani ya Mkoa wa Kigoma kama Samaki, Dagaa, Mazao ya chakula na yale ya Biashara’’ amesema.
Kupitia Kikao hicho, Mkuu wa Mkoa amewaelekeza wakuu wa Idara, Seksheni na Taasisi mbalimbali za Kiserikali kuhakikisha mahitaji yote ya muhimu yatakayowezesha ujenzi wa chuo hicho yanapatikana na na kufika eneo la ujenzi kwa wakati.
‘’Hatutarajii Taasisi za Serikali kukinzana katika kutekeleza zoezi la kufikisha Miundombinu muhimu kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa chuo. Shirikianeni na kuhakikisha Maji, Umeme, mawasiliano na Barabara vinafika katika eneo husika bila kuwepo kwa sababu zozote za ucheleweshaji kwa kuogopa kuharibu miundombinu mingine’’ Amesisitiza Andengenye.
Akitoa Taarifa ya uanzishwaji wa mradi wa Kampasi hiyo, Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Rehema Horera amesema mradi wa Ujenzi wa Kampasi ya MUHAS utatekelezwa na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Tranformation)
Ameyataja Malengo ya Mahususi ya Mradi wa HEET kuwa ni kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika Taasisiza Elimu ya Juu, kuwaimarisha kitaaluma wahadhiri wa vyuo vikuu, kuboresha mifumo ya TEHAMA na Mitaala ya Elimu ya juu.
‘’Lengo lingine muhimu la Mradi huu ni kuboresha mitaala mia nne ya Elimu ya Juu nchini ili Mwanafunzi atakayemaliza Elimu ya Chuo Kikuu aweze kujiajiri au kuajirika kwa urahisi kutokana na kuwa na muelekeo toshelevu wa kiujuzi’’ amesema Dkt. Horera.
Naye Mratibu wa Mradi wa HEET-MUHAS Prof. Erasto Mbungi amesema Mradi huo utakapokamilika sambamba na Ujenzi wa Hospitali Kuu ya Kanda, utapunguza Adha ya wananchi kwenda katika Hospitali kubwa zilizo nje ya Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya kufuata huduma za matibabu za kibingwa.
Upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Godfrey Smart ameishukuru Serikali kwa kuuelekeza Mradi huo mkoani Kigoma kwani utaongeza idadi ya wataalam pamoja na kuimarisha matibabu ya kisasa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa