KATIBU TAWALA WA MKOA WA KIGOMA ALBERT MSOVELA AKIZUNGUMZA NA WATUMISHI WA UMMA KATIKA HALMASHAURI YA MJI WA KASULU(HAWAPO PICHANI) IKIWA NI MUENDELEZO WA ZIARA YAKE YA KUZUNGUMZA NA WATUMISHI WA UMMA KATIKA HALMASHAURI NANE ZA MKOA WA KIGOMA.
Watumishi wa Umma mkoani Kigoma wametakiwa kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kazi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuharakisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi katika Jamii.
Akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Albert Msovela amesema ni muhimu kwa watumishi kuwa na Ushirikiano ili kuchochea uboreshaji wa utoaji wa Huduma kwa Wananchi.
Amesema baadhi ya watumishi wa Umma hutumia muda mwingi kuvutana na kusengenyana hali inayochochea migogoro katika maeneo ya kazi badala ya kutekeleza majukumu yao ya kiutumishi huku wakisababisha wananchi kukosa huduma za kuridhisha.
‘’Kama hakuna umoja, mshikamano, kuheshimiana na kuzingatia mtitiriko wa mipango kazi inayowekwa na Serikali, hatuwezi yetu na matokeo chanya ya mipango hiyo hayataweza kupatikana’’ amesema.
Ninaamini pamoja na uwepo wa Sheria na taratibu za kiutumishi, kama hakuna upendo miongoni mwetu, nidhamu ya kazi, kujitolea na kujituma, daima itakuwa vigumu kuleta tija katika utendaji wetu.
‘’Nasisitiza mfanye vikao vya mara kwa mara vitakavyohusisha Idara na vitengo, vikao vya kisheria vya Halmashauri, mkutane na wadau wenu wa Maendeleo pamoja na kushirikishana katika maamuzi mbalimbali pamoja na usimamizi wa miradi inayotekelezwa katika Halmashauri’’ amesisitiza.
Aidha Katibu Tawala huyo amewaasa watumishi hao kuongeza nguvu katika usimamizi wa mapato ya ndani ili kuiwezesha Halmashauri kujiendesha.
‘’Ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mfumo wa Tausi iwe Agenda ya msingi kila mtakapokutana ili kuimarisha makusanyo ya ndani’’ alisisitiza Msovela.
Naye Mhasibu Mkuu wa Mkoa Johnson Gamba amewasisitiza watumishi hao kujenga nidhamu ya matumizi ya Fedha huku wakizingatia Kanuni na Taratibu zinazoongoza matumizi ya Fedha za Umma.
Aidha kupitia wasilisho lake kwa watumishi hao, Gamba amemwelekeza Mkurugenzi na Mweka Hazina kutekeleza majukumu yanayohusu matumizi ya fedha kwa kuzingatia uwazi na ushirikishwaji wa watumishi wanaohusika na matumizi hayo.
Upande wake Zainab Mkamba ambaye ni Afisa Utumishi na Rasilimali watu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, ametoa wito kwa watumishi hao kuzingatia maadili na taratibu za kiutumishi.
‘’Tunahudumia jamii hivyo tuzingatie tabia na mienendo inayozingatia miongozo ya kiutumishi ili tuweze kuwa mfano kwa jamii’’ amesisitiza Zabibu.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa