KATIBU TAWALA MKOA WA KIGOMA ALBERT MSOVELA AKIZUNGUMZA NA WASHIRIKI WA KIKAO CHA KAMATI YA MSINGI YA AFYA MKOA WAKIGOMA (HAWAPO PICHANI) KILICHOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA OFISI YA MKUU WA MKOA WA KIGOMA SEPTEMBA 8, 2023. KUSHOTO KWAKE NI MGANGA MKUU WA MKOA WA KIGOMA DKT. JESCA LEBBA.
WASHIRIKI WA KIKAO CHA KAMATI YA MSINGI YA AFYA MKOA WA KIGOMA WAKIFUATILIA JAMBO WAKATI WA KIKAO.
Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya magonjwa kwa kuzingatia kanuni za Afya pamoja na kushirikiana na Serikali kupitia wataalam wa Afya ili kupambana na kudhibiti maradhi mbalimbali yanayojitokeza katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa Kigoma Albert Msovela alipofungua mafunzo kwa Kamati ya Msingi ya Afya Mkoa, yaliyolenga kuijengea uwezo katika kutoa Elimu kwa Jamii kuhusu Kampeni ya utoaji chanjo ya Polio inayotarajia kuanza kutekelezwa mkoani hapa Septemba 21 hadi 24, 2023.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imebaini na kuthibitisha uwepo wa ugonjwa wa Polio katika baadhi ya maeneo nchini pamoja na nchi jirani, hali iliyosababisha ichukue hatua za makusudi kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa huo.
Amesema tayari serikali imetoa chanjo 1,105,000 kwa ajili ya kuchanja na kutoa kinga kwa watoto wote walio na umri chini ya miaka nane kwa mkoa wa Kigoma, ambapo zoezi hilo litafanyika nyumba kwa nyumba, kupitia vituo vya kutolea Huduma za Afya, Shuleni pamoja na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu.
Amesisitiza kuwa, ili kufanikisha malengo ya kampeni hiyo, kila Mwananchi anapaswa kushiriki kuwasaidiia watoa huduma katika kuwabaini walengwa wote ili waweze kufikiwa na kupatiwa chanjo hiyo.
Aidha Msovela ametoa Rai kwa wakazi mkoani hapa kuendelea kuzingatia kanuni za Usafi ikiwemo kunywa maji safi na salama pamoja na kutumia vitakasa mikono kwa lengo la kuepuka na kudhibiti uwezekano wa kuibuka na kuenea kwa maradhi ya tumbo.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba amesema wataalam wa Afya wanaendelea kukabiliana na kuchukua hatua za kitabibu dhidi ya wahisiwa wa maradhi ya Surua pamoja na waliobainika kuwa na maradhi ya kuhara katika wilaya ya Kibondo mkoani hapa.
Aidha amesisitiza kuwa, kutokana na muingiliano wa Raia kutoka nchi jirani, wakazi wenyeji wanatakiwa kuchukua tahadhari na kutoa taarifa mapema wanapobaini dalili za uwepo wa Maradhi mbalimbali katika maeneo yao.
Akiwasilisha mada kwa Kamati hiyo, Mratibu wa chanjo Mkoa wa Kigoma Yohanes Mwitanyi amezitaja njia za kujikinga na maradhi ya Polio ikiwa ni pamoja na kutakasa mikono nyakati zote, kutumia vyoo, kunywa maji safi na salama, kula chakula kilichoandaliwa kwa usafi pamoja na kuosha vyakula kabla ya kula.Mratibu huyo wa chanjo amewataka washiriki wa kikao hicho kuwa mabalozi wazuri wa chanjo ya Polio kwa kuuelimisha Umma kuhusu Usalama wa chanjo hiyo na umuhimu wake ili kumuepusha mtoto dhidi ya ulemavu unaosababishwa na kupooza ghafla kwa viungo vya mwili.
‘’Niwaombe kwa nafasi zenu, ukiwa kiongozi wa dini, mwakilishi wa mashirika binafsi, kiongozi katika taasisi za Umma, wataalam pamoja na wanahabari, sote tutumie majukwaa tunayoyafikia kufikisha ujumbe huu muhimu kwa jamii ili iweze kujenga utayari na muitikio chanya kuhusiana na zoezi hili ili liweze kufanikiwa kwa asilimia mia mkoani kwetu’’ amesisitiza Mwitanyi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa