Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Albert Msovela amewakumbusha watumishi wa Umma katika Halmashauri za Mkoa wa Kigoma kuzingatia kanuni na taratibu za manunuzi Serikalini ili kuepuka kusababisha Hoja za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali zinazoweza kuepukika.
Msovela ametoa wito huo Leo Juni 8, 2023 alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani wa wilaya ya Uvinza lililoketi kwa lengo la kupokea na kupitia Taarifa ya Majibu ya Hoja, Utekelezaji pamoja Mapendekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2021/2022.
Amesema Serikali imeweka Kanuni na Taratibu za Manunuzi ili kuhakikisha kunakuwepo na ukweli na uwazi katika matumizi ya Fedha za Umma, hivyo wanaosimamia na kutekeleza jukumu hilo katika Halmashauri, wanatakiwa kulisimamia kwa dhati ili kuzuia uwezekano wa kuibuka kwa hoja za kiukaguzi ambazo kimsingi zinaweza kuepukwa.
Aidha Katibu tawala ameziagiza Menejiment katika Halmashauri za Mkoa wa Kigoma kuimarisha usimamizi wa makusanyo, matumizi ya masurufu pamoja na michakato yote Manunuzi ili kudhibiti kuibuka kwa hoja za ukaguzi ambazo zimekuwa zikijirudia mara kwa mara.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani amesema ataendelea kushirikiana na wataalam ili kuhakikisha hoja zilizobainika zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na kuhakikisha Halmashauri ya Uvinza inaendelea kupata Hati Safi katika kila zoezi la Ukaguzi wa Hesabu za Serikali.
Mathamani ameahidi kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na watendaji kwa lengo la kubaini, kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zilizobainishwa kwenye taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.
Kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza ilipata hati Safi ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa