Watendaji wa Serikali katika ngazi za Halmashauri mkoani Kigoma wameshauriwa kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi kabla na wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo inayotokana na fedha kutoka kwa wafadhili ili kuifanya miradi hiyo kuwa endelevu.
Ushauri huo umetolewa na Dkt. John Lusingu Mshauri wa masuala ya kielimu katika ubalozi wa Uingereza nchini, alipozungumza akiwa katika ziara ya kukagua na kufanya Tathimini ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo inayotekelezwa chini ya programu ya Shule Bora wilayani Buhigwe mkoani hapa.
Amesema watendaji katika ngazi za halmashauri hususani Mkurugenzi kwa kushirikiana na wataalam kutoka Idara ya Elimu, wanapaswa kukaa na kuwahusisha wananchi hatua zote za utekelezaji wa miradi hiyo kwani hupelekewa katika maeneo yao ikiwa na mipango kazi ambayo watekelezaji wakuu ni wananchi.
Amefafanua kuwa, Miradi yote huja na mipango kazi hivyo walengwa wanapokuwa na uelewa kuanzia kwenye mipango kazi hadi utekelezaji wake, huifanya miradi hiyo iweze kudumu kutokana na wao wenyewe kumudu kuiendesha, jambo litakalosaidia iweze kuwanufaisha kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.
Kupitia ziara hiyo, Dkt. Lusingu amesema ameshuhudia mapinduzi na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa mradi wa Shule Bora wilayani Buhigwe ambapo shule zinazotekeleza mradi huo zimeweza kuibua shughuli za uzalishaji mali ikiwemo upandaji wa misitu na baadhi ya shule hizo zikiwa zimefanikiwa kuivuna misitu hiyo na kutumia fedha zilizopatikana kwa ajili ya kuanzisha miradi mingine ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu.
Ameyataja mafanikio mengine yaliyofikiwa wilayani Buhigwe kuwa ni uanzishwaji wa kilimo cha zao la Kahawa, Ufugaji wa nyuki, kuku, sambamba na miradi mbalimbali na kuwa vyanzo vya mapato katika shule hizo.
Mwalimu Judith Ndiga wa Shule ya Msingi Mkatanga, amesema utekelezaji wa Mradi wa Shule Bora kupitia Programu ya UWAWA, umefanikiwa kuanzisha utaratibu wa kudumu kwa ajili ya kutoa chakula kwa wananfunzi shuleni hapo, jambo linalosaidia katika kuongeza ufanisi wa kitaaluma na kupunguza utoro.
‘‘Utaratibu huu wa kuwapatia wanafunzi wetu chakula hapa shuleni umesababisha waweze kujenga tabia ya kufika shuleni bila msukumo wowote wa wazazi au walimu, aidha utaboresha kiwango cha ufaulu sambamba na kuimarisha Afya za watoto’’ amesisitiza Mwalimu Judith.
Upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mnyegera iliyopo wilayani Buhigwe Fidel Ernest amesema mara baada ya kuanza utekelezaji wa programu ya mafunzo endelevu ya walimu kazini(MEWAKA) hali ya kujiamini kwa walimu kiufundishaji imeongezeka sambamba na ongezeko la ufaulu hadi kufikia zaidi ya Asilimia 90 kwa Mwaka 2023.
Aidha Mwalimu Ernest amesisitiza kuwa maboresho makubwa yay a miundombinu ya kielimu yanayofanywa na serikali kupitia mradi huo, yameendelea kuyafanya mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kuwa rafiki kwa walimu pamoja na wanafunzi hali inayoendelea kuimarisha utoaji wa elimu yenye ubora kwa watoto.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa