Shughuli mbalimbali za kibinadamu zinaelezwa kuwa ndicho chanzo kikubwa cha mabadiliko ya Tabianchi huku zikisababisha uzalishwaji mkubwa wa Hewa Ukaa ambayo huathiri mwenendo wa hali ya hewa na kusababisha mafuriko, ukame, joto kali, baridi iliyopitiliza, vimbunga na hata kuhatarisha usalama wa maisha ya viumbe hai.
Namna bora ya kukabiliana na mabadiliko hayo ni kudhibiti uharibifu wa misitu ya Asili iliyopo na kuongeza kasi katika upandaji wa misitu mipya na kuitunza, kwani uwepo wake umethibitishwa na wataalam wa Mazingira kufyonza hewa ukaa inayosababishwa na kazi mbalimbali za uzalishaji zinazopelekea uchafuzi wa mazingira.
Mpango wa udhibiti wa Hewa ukaa kupitia misitu sambamba na kuongeza ufanisi katika mchakato wa utunzaji wa Mazingira, kwa Mujibu wa Chapisho la Gazeti la Habari Leo Feb 15, 2021, hii ni biashara iliyothibitisha kuwainua kiuchumi wakazi wa Katavi kwa kufanikiwa kuuza Tani 82,000 za Hewa hiyo kwa Thamani ya Shilingi 250,000,000.
Kupitia chapisho hilo, Fedha zinazopatikana sambamba na kuwanufaisha wananchi zimekuwa zikitumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo kama ujenzi wa miundombinu ya kielimu, Afya na kusogeza nishati ya Umeme.
Serikali ya Mkoa wa Kigoma imefanikiwa kutia saini katika utekelezaji wa Awali wa Mkataba wa kuanza kwa mradi huo utakaosimamiwa na kuratibiwa na Kampinu ya Ørsted Nature Based Solution A/S kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia wakimbizi la Denmark (DRC).
Biashara hii itaanza kufanyika katika Halmashauri za Wilaya Kakonko, Kibondo na Kasulu ambapo kwa sasa utambuzi na upembuzi yakinifu uliolenga kubaini maeneo hitajika umeshafanyika na hatua iliyobaki ni kukutana na wananchi kwa ajili ya kuwapa elimu, kuridhia utoaji wa maeneo ya vijiji hususani yale yanayomilikiwa na Serikali pamoja na kuingia mikataba rasmi kwa ajili ya kuanza kwa zoezi hilo.
Maisha ni kupanga na kuchagua, jukumu la wananchi hususani katika maeneo yaliyotambuliwa ni kuhakikisha wanaunga mkono mpango huu bila kuingiza mivutano isiyo na tija kwa mustakabali wa maendeleo yao binafsi pamoja na Halmashauri walizopo. Ifahamike kuwa zoezi la uanzishaji wa Mradi huu ni shirikishi na uhalali wa utekelezaji wake utategemea ridhaa ya wananchi.
Sambamba na manufaa kiuzalishaji, shughuli za kibinadamu kupitia viwanda husababisha athari kubwa ya za kimazingira kupitia hewa hiyo na madhara yake tunaendelea kuyashuhudia kila uchao hivyo hatuna budi kuunga mkono juhudi za serikali kwa kushirikiana na wadau ili sote tuweze kutunza mazingira ambayo ni urithi wetu wa Asili kwa lengo la kujipatia mkate wa kila siku kupitia mauzo ya hewa hiyo ambapo hatutolazimika kibarua cha kututoa jasho kufikia uzalishaji.
Ni jukumu la kila mkazi hususani katika maeneo yatakayopata fursa ya kuguswa na mradi huo kuitumia fursa hiyo sambamba na kutunza mazingira bali kujikusanyia ukwasi kwa ajili ya kumudu gharama za maisha na kuleta maana halisi ya lengo la serikali katika kumuinua mwananchi kiuchumi.
Rai yangu kwa wakazi ni kushiriki vikao vya maamuzi vitakavyowakutanisha na wataala wa mradi katika maeneo yao ili waweze kujengewa uelewa wa kina kuhusu hatua za utekelezaji na faida za mradi badala ya kusubiri tetesi kutoka kwa wapinga maendeleo kupitia porojo za vinywa vyao.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa