Awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara ya Mwandiga, Chankere, Mwamgongo, Kagunga katika Halmashauri ya Kigoma, mkoani Kigoma kipande chenye urefu wa Km. 20 umefikia asilimia 95 na tayari imeanza kutumika na kuwaondolea kero ya usafiri wakazi katika maeneo hayo ambapo awali usafiri pekee uliokuwa ukitumika kuyafikia maeneo hayo kutoka mjini Kigoma ni ule wa njia ya Maji katika Ziwa Tanganyika.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali. Michael Ngayalina ametoa wito kwa wakazi katika maeneo hayo kutumia fursa ya ujenzi wa barabara hiyo kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi kwa kusafirisha bidhaa mbalimbali za kilimo na uvuvi ili kuyafikia masoko kwa haraka.
Amesema barabara hiyo ya kwanza kujengwa tangu nchi kupata Uhuru, imekuwa chachu kubwa ya kuimarisha utoaji wa huduma sambamba na kuwaondolea adha ya usafiri ambapo kwa sasa badala ya kutembea kwa miguu na kutumia njia za maji, wakazi watatumia magari na pikipiki.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma Mha. Mwita Joram amesema Mradi unatekelezwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Barabara (Road Funds) kwa Thamani ya Shilingi Bil.3 ambapo ujenzi wake ulianza Desemba 14, 2024 huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025.
Fausta Athanasi Mkazi wa Kijiji cha Mwamgongo amesema awali wakina mama wengi walikuwa wakijifungulia nyumbani kutokana na changamoto ya ukosefu wa barabara.
Aziz Segeje mkazi wa kitongoji cha Mgazo katika kijiji cha Mwamgongo amesema mara baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo, wakazi wanasafiri na kusafirisha biashara zao kwa wepesi na gharama nafuu hususani kwa kutumia usafiri wa pikipiki badala ya kutegemea usafiri wa njia ya maji pekee.
Amesema ujenzi huo wa barabara umeweza kuwaondolea kero ya kusafirisha wagonjwa kwa kutumia machela ili kuwafikisha kwenye vituo jirani vya kutolea huduma za Afya.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa