Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti amewataka maafisa Uvuvi mkoania Kigoma kuongeza kasi katika kudhibiti kuenea kwa zana haramu za uvuvi kabla ya kuwafikia wananchi ili kuwaepushia hasara kutokana na hizo kukamatwana kuteketezwa na serikali.
Mnyeti ametoa kauli hiyo alipozungumza kwenye hafla ya kukabidhi boti tisa za Uvuvi kwa wanufaika mkoani Kigoma huku akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuimarisha uchumi wa wananchi kwa kuhamasisha na kuongeza tija katika uzalishaji kupitia mazao ya Samaki.
Naibu waziri huyo amewaelekeza maafisa uvuvi kufuatilia na kuhakikisha wanafunga maduka na kuwakamata wafanyabiashara wote wanaouza nyavu ambazo kisheria haziruhusiwi kutumika kwa shughuli za uvuvi nchini.
‘’Nendeni mkafanye msako katika maeneo yote yanayozalisha, kuuza na kufanya matumizi ya zana haramu za uvuvi na kuzidhibiti ili zisitumike katika mito, mabwawa, maziwa na bahari zetu’’ ameagiza Mnyeti.
Naibu waziri huyo amewakumbusha watendaji hao wa serikali kutekeleza wajibu wao wa kutoa Elimu na miongozo ya uvuvi bora badala ya kusubiri wavuvi wafanye makosa kisha kuwatoza fedha kutokana na makosa hayo, hali inayosababisha baadhi yao kufilisika.
‘’Baadhi yenu mmegeuka wakusanya mapato wa Halmashauri badala ya kusimamia majukumu yenu ya msingi ya kutoa elimu na kusimamia taratibu za uvuvi’’ amesisitiza Mnyeti.
Baadhi ya wanufaika wa zana hizo za uvuvi zilizotolewa kwa njia ya mikopo nafuu kutoka serikalini wamesema wanauhakika wa kurejesha mikopo yao kutokana na vyombo hivyo kutumia mifumo ya kisasa katika mchakato wa uvuvi.
Amesema ziwa Tanganyika linasamaki wengi lakini changamoto iliyokuwa ikiwakabili ni kukosa zana za kisasa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya uvuvi.
Jumla ya boti Tisa zenye Thamani ya Shilingi Mil.535 zimekabidhiwa kwa vikundi vya wanufaika katika Halmashauri ya Kigoma, Uvinza na Manispaa ya Kigoma Ujiji.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa