Mkoa wa kigoma umenuia kuwa kinara wa kilimo cha zao la chikichi na kuzalisha bidhaa mbalimba zitokanazo na zao hilo kwa kuanzisha mpango kazi kabambe na mikakati ya kilimo cha chikichi.
Uongozi wa Mkoa wa Kigoma umeandaa mpango wa kuendeleza zao la chikichi unaozingatia kunua zao hili ili liwe sehemu kubwa ya bidhaa ghafi katika kufanikisha adhma ya viwanda vya Mkoa kuanzisha kiwanda cha kuchakata mawese.
Takwimu zinaonesha kuwa mwaka wa 2000 hadi 2007 zaidi ya 95% ya mafuta ya kula yaliyoagizwa nchini yalikuwa ni mawese. Pia takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka wa 2016, mahitaji ya Taifa ya mwezi ya mawese yalikuwa ni tani 50,000, wakati uzalishaji wa mafuta haya kwa mwaka ni tani 40,000 zikiwemo tani 30,000 zinazozalishwa na Mkoa wa Kigoma
Kutokana na takwimu hizi ni dhahiri kuwa uzalishaji wa mafuta ya mawese haukidhi mahitaji ya Taifa ambayo ni tani 600,000 kwa mwaka ikiwa ni upungufu wa tani 560,000.
Uagizaji wa mafuta ya mawese umeongezeka kutoka tani 3,000 mwaka wa 1978 hadi tani 510,000 mwaka jana 2016 na utaongezeka kwa miaka ijayo.
Aidha utumiaji wa fedha za kigeni kuagiza mawese kutoka nje umeongezeka kutoka dola za kimarekani 13,000,000 mwaka 1961 hadi zaidi ya 320,000,000 kwa mwaka wa 2016.
Kigoma ni Mkoa pekee unaolima zao la michikichi kwa wingi nchini Tanzania ukiwa na hekta 18,924 zenye michikichi inayozalisha tani 30,010 ambayo ni tani 1.6 kwa hekta za matunda ya chikichi. Uwezekano wa uzalishaji ni tani 75,700 sawa na tani 4.0 kwa hekta kwa eneo lililopo lenye michikichi.
Hali ya uzalishaji wa chikichi Kigoma kwa sasa inaonekana kuwa bado ipo chini kwa sababu uzee wa michikichi iliyopo, mashamba kutokutunzwa kitaalam, ukosefu wa mbegu bora pamoja na teknolojia duni ya uchakataji wa zao hilo.
Mpango wa Mkoa unalenga kuwa na viwanda 7 vya kisasa vya kusindika malighafi itakayozalishwa, Kiwanda kikuu kimoja kitakachoweza kusindika mawese ghafi, Viwanda vidogo vinne vitawekwa kwenye vijiji vitakavyopendekezwa na MSM, Kiwanda kimoja kwa ajili ya usindikaji wa mafuta ya alizeti. Baada ya miaka kadhaa, Mkoa unatarajia kujenga kiwanda cha kutengeneza gesi kutokana na mashudu ya michikichi.
Ili kuongeza tija ya zao la chikichi Mkoa unahamasisha wilaya zote zenye maeneo yanayofaa kwa kilimo cha chikichi, kufufua mashamba na kuanzisha mapya. Pamoja na kuvutia makampuni binafsi kuzalisha miche bora na kuisambaza kwa wakulima.
Mpango wa kuinua zao la chikichi Kigoma umepanga kuanza na wakulima 100,000 ambao watapewa mbegu
zilizoboreshwa (chotara) kila mmoja miche 150 ambayo itatosha kupanda eneo la hekta moja ekari mbili na nusu.
Kwa sasa mbegu bora hazipatikani nchini kwetu bali zinaagizwa kutoka nchi kama Costa Rica, Malaysia na Indonesia kwa gharama ya dola ya kimarekani moja kwa mbegu moja.
Njia mbadala ambayo Mkoa umepanga ni kuwa na kituo chake cha uzalishaji mbegu na maabara. Hiki kituo kitafanya utafiti na uzalishaji wa miche bora kwa kutumia mfumo wa kisasa ili kuzalisha miche mingi kwa gharama ndogo na kwa muda mfupi.
Uongozi wa Mkoa wa Kigoma unaona kuna umuhimu wa zao la chikichi kuwa na bodi ya zao la chikichi ili kusaidia uendelezaji wa kilimo cha zao hilo. Aidha, wananchi wabadilishwe mtazamo juu uendelezaji wa zao la chikichi. Wananchi wahamasishwe ili wajiunge na walime kupitia vyama vya ushirika.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa