Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ahimiza uwekezaji katika viwanda vidogovidogo.
Posted on: June 20th, 2017
Sekta binafsi na Sekta ya Umma Mkoani Kigoma zimetakiwa kushirikiana katika kutengeneza mazingira bora ya kibiashara na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje. Akizungumza katika Mafunzo ya siku mbili ya Majadiliano ya pamoja kati ya Sekta binafsi na sekta ya Umma, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Brigedia Jenerali (mst.) Emanuel Maganga alisema, ili kuwepo na mazingira mazuri ya kibiashara, kunahitajika mashirikiano ya karibu kwa wadau mbalimbali hususan sekta binafsi na sekta ya umma ili kuangalia namna gani ya kuimarisha mazingira rafiki kwa biashara na kuvutia wawekezaji wa nje na ndani.
aliongeza kuwa kuna sababu nyingi za kifursa Mkoani Kigoma ikiwemo hali ya hewa nzuri, jiografia yenye fursa, madini, utalii, ardhi yenye rutuba na Ziwa Tanganyika. Hizi ni fursa kubwa katika biashara zikitumiwa ipasavyo uchumi wa Mkoa wa Kigoma utapaa.
Ameziagiza Halmashauri zitengeneze mipango mikakati ya namna ya kuweka miundombnu mizuri ya kibiashara ikiwemo kutenga maeneo ya uwekezaji. Alisema nchi yeyote haiendelei kwa kuwa na rasilimali tu bali uwepo wa mipango mathubuti na wataalam wanaoweza kushauri namna bora ya kutumia rasilimali hizo. Tuchangamkie furasa hii, kwa kunadi fursa zilizopo Mkoani Kigoma.
Ametoa wito kwa mashirika mbalimbali na Taasisi binafsi kuanziasha viwanda vidogovidogo ambavyo havihitaji gharama. Aidha amewataka wafanyabiashara wafanye biashara halali na kuzingatia sheria za nchi hasa ulipaji wa kodi.
Mafunzo hayo yalifanyika chini ya ufadhili wa TCCI, BEST, na LIC kwa lengo la kujadili na kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya biashara Mkoani Kigoma na namna ya kushirikiana kati ya sekta binafsi na sekta ya umma kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji.