Mkuu waa Mkoa wa Kigoma Brig. Gen. Emmanuel Maganga amesema haridhishwi na utendaji kazi wa maafisa wanaoshughulikia Malarai Mkoani Kioma na kwamba wajitathmini kabla ya kuanza kuchukuliwa hatua za kushindwa kusimamia majukumu yao, kwani badala ya kushuka kwa takwimu za maambukizi ya malaria Mkoani Kigoma, badala yake kunaongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo.
Mkuu wa Mkoa amesema haya wakati akizundua kampeni ya ugawaji wa vyandarua kupitia shule shule za msingi, amesema takwimu za sasa zinaashiria ukubwa wa tatizo la malaria katika mkoa kuwa juu, ukilinganisha na mikoa mingine. Hali hii inajidhirisha katika takwimu za Viashiria vya Ugonjwa wa malaria kwa Watoto chini ya miaka 5 ya mwaka 2017 ambapo kigoma ilionekana kuwa na asilimia 24.4, kiwango cha juu kuliko mikoa yote Nchini huku wastani wa Kitaifa ikiwa ni asilimia 7.3%
Amesema kasi ya mapambano ya malaria kwa Mkoa wa Kigoma inaonekana ipo chini na hivyo kutishia kutofikia kwa Malengo ya kutokomeza ugonjwa huo. Kutokana na hali hii amewaambia Maafisa wanaohusika na program ya utokomezaji wa Malaria kwa kila Wilaya kujitathmini na kibidi waachie nafasi hizo kabla ya kuchukuliwa hatua. Natoa agizo kwa viongozi wote kuanzia ngazi ya Mkoa na Halmashauri kuhakikisha afua za kupambana na Malaria zinakuwa ni ajenda ya vikao vyote vya maamuzi na utekezaji wa afua hizi upimwe kila mwezi kuanzia leo hii ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Awali akitoa taarifa Mganga Mkuu wa mkoa wa Kigoma Dkt. Paul Chaote amesema takwimu kutoka vituo vya kutolea huduma za afya mwaka 2017 Mkoani Kigoma zinaonesha kuwa asilimia 33.5 ya wagonjwa waliohudhuria kupata huduma za nje (OPD) walikutwa na ugonjwa wa malaria na mwaka 2018, asilimia 29.2. Vivyo hivyo katika mwaka 2019, hadi mwezi wa 6, asilimia 28.98 ukilinganisha na magonjwa mengine.
Malengo ya mapambano dhidi ya malaria nchini Tanzania ni kupunguza kiwango cha malaria kufikia chini ya asilimia 1 ifikapo mwaka 2020 na hatimaye kutokomeza malaria ifikapo 2030.
Tayari hatua za kupambana na ugonjwa huo mbaya zimeanza kwa kuzindua kampeni ya ugawaji vyandarua ya Ugawaji wa vyandarua kwa wajawazito, Watoto wa miezi 9 kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na Kupitia wanafunzi wa shule ya Msingi na zoezi la unyunyiziaji wa viuadudu kwenye mazalia ya mbu.
Imeelezwa kuwa hadi sasa Mkoa wa Kigoma umepokea kiasi cha lita 7616 za viududu vya kibaiologia kutoka Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo tayari vimesambazwa katika Halmashauri zote 8 za mkoa wa Kigoma ambapo Jumla ya Majengo 248,000 yanatarajiwa kupuliziwa
Maandalizi ya Upuliziaji wa Kiuatilifu Cha Ukoko Majumbani yameanza ambapo mwaka huu zoezi hili litafanyika katika halmashauri za wilaya za Kakonko, Kibondo na Kasulu, pamoja na kuhusisha kambi za wakimbizi zote tatu. Lengo la zoezi hili ni kupunguza kiwango cha malaria kwa kiasi kikubwa na kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa