Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameshuhudia utiaji saini Mikataba Mitatu ya Ujenzi ikihusisha Kiwanda cha ujenzi wa Meli na Meli Mbili za mizigo baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Diarshan Shipyard ya Nchini Uturuki.
Hafla hiyo ya Utiaji saini imefanyika katika Bandari ya Kigoma ambapo mikataba hiyo yenye Thamani ya zaidi ya Bil. 600 Itahusisha ujenzi wa kiwanda hicho mkoani Kigoma, Meli mbili za mizigo zitakazohudumu ziwa Tanganyika na ziwa victoria.
Akizungumza katika Hafla hiyo, Waziri Mbarawa amesema karakana hiyo itakuwa na vifaa vya kisasa na kwa kuanza inatarajia kuwezesha utengenezaji wa Meli yenye uwezo wa kubeba mizigo hadi kufikia Tani 3500 itakayotumika ziwa Tanganyika pamoja na Meli ya Tani 3000 itakayotumika Ziwa Victoria.
Ameendelea kueleza kuwa Meli itakayojengwa mkoani Kigoma itakuwa na uwezo wa kusafiri kutoka Bandari ya Kigoma hadi Kalemi Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo kwa kutumia Masaa Sita.
Awali akitoa Salama za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesema maboresho makubwa ya miundombinu yanayoendelea kufanywa na Serikali yataendelea kurahisha michakato ya usafirishaji wa bidhaa , kuimarisha huduma za kibiashara pamoja na kuongeza fursa za uwekezaji mkoani Kigoma.
Amesisitiza wananchi kuendelea kutumia fursa hizo kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja pamoja na Taifa kwa ujumla.
Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bandari nchini Erick Hamis amesema uwekezaji katika ujenzi wa kiwanda cha Ujenzi wa Meli unatarajiwa kuleta Mapinduzi katika Tasnia ya ujenzi wa Meli nchini.
Amesema kuwa Kiwanda hicho kitakuwa cha kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo pia kitatoa fursa za kutoa huduma za ujenzi wa Meli katika nchi jirani za Congo, Burundi na Zambia.
Aidha Hafla hiyo imehudhuriwa na Mabalozi kutoka nchi za Burundi na Congo, Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kigoma, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Kamati ya Usalama Mkoa, wabunge, viongozi wa Dini na vyama vya Siasa pamoja na wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Serikali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa