Viongozi wa Madhehebu Dini nchini wametakiwa kuimarisha Mafunzo ya Maadili kwa wanandoa kutokana na vitendo vingi vya ukatili na unyanyasaji kufanyika katika ngazi ya Familia na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa maadili katika Jamii.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju alipofungua warsha ya Viongozi wa Dini wa Mikoa mitano ya Tanzania Bara iliyofanyika Mkoani Kigoma leo Agosti 7, 2023.
Amesema uwepo wa migogoro ndani ya ndoa pamoja na wazazi wengi kutokutekeleza kwa ufasaha majukumu yao ya kimalezi kwa watoto wao, kumeendelea kusababisha kuibuka kwa wimbi kubwa la Tabia na mienendo isiyoridhisha miongoni mwa wanajamii.
‘’Katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara tumeamua kuanda mwongozo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini ili kutoa Dira kwa wazazi na jamii kwa ujumla itakayowapa mwelekeo ili kupata namna bora ya kutoa malezi kwa watoto’’ amesisitiza Mpanju.
Aidha Kiongozi huyo amesisitiza uwepo wa umakini katika matumizi ya Teknolojia na Utandawazi ikiwemo kudhibiti mafunzo na uigizwaji wa tabia zinazoenda kinyume na Mafundisho ya kiimani pamoja na Mila na Desturi za kiafrika.
Naye Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mustapha Rajabu amesema jamii inapaswa kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yatakayowaimarisha kimwili na kiroho na kuwafanya waishi maisha yenye uadilifu.
‘’Malezi kwa watoto wetu yaendane na upendo, upatikanaji wa Huduma ya Elimu Dini na ile ya kidunia pamoja na uadilidhwaji mkubwa kuhusu namna bora ya kuishi’’ amesisitiza Shehe Rajabu.
Upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Kigoma Joseph Mlola ameishukuru Wizara kwa hatua inazoendelea kuchukua kwa lengo la kurejesha misingi ya Maadili katika Jamii.
Aidha mlola amewasisitiza wajumbe wa kikao hicho kufuatilia kwa ukaribu mada mbalimbali zitakazotolewa kisha kutoka na mapendekezo yatakayoleta mabadiliko yenye tija kwa Taifa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa