Katika kuhakikisha Kilimo kinaendelea kuwa Muhimili muhimu wa kiuchumi mkoani Kigoma, Bodi ya Kahawa nchini kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) wanatarajia kuzalisha miche ya mbegu bora ya Kahawa Mil. 4.5 na kuigawa bure kwa wakulima wa zao hilo mkoani hapa katika msimu wa Kilimo wa Mwaka 2023/2024.
Hayo yamebainishwa na Afisa Ugani na Msimamizi wa Mradi wa Kitalu cha Miche bora ya Kahawa kilichopo kata ya Kalinzi wilayani Kigoma, Richard Nelson alipotoa taarifa ya utekelezaji kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 alipotembelea na kukagua mradi huo.
Ameeleza kuwa, hadi kufikia mwaka 2026 kilimo cha zao hilo kitaongezeka maradufu mkoani Kigoma kutoka Hekta 1500 zinazolimwa sasa na kufikia Hekta 3000 kutokana na kuongezeka kwa eneo la uzalishaji, kutakakosababishwa na ongezeko la upatikanaji wa miche ya bure.
Amesisitiza kuwa sambamba na wananchi kutarajiwa kunufaika kiuchumi kutokana na ongezeko la uzalishaji, Kilimo cha zao hilo kitaongeza makusanyo ya ndani ya Halmashauri ya Kigoma na kuimarisha uwezo pamoja na fursa ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.
Miche hiyo inatarajia kuwa mkombozi kwa mkulima kutokana na kuwa na ongezeko la Tija katika uzalishaji ikilinganishwa na iliyopo sasa ikiwa na uwezo wa Tani 1 huku mbegu mpya ikizalisha tani 1.5 kwa Mwaka.
Mradi huo wenye Thamani ya Shilingi Mil. 750, unatarajia kuanza kugawa miche hiyo kwa wakulima wa Kahawa wilayani humo kuanzia mwanzoni mwa Mwezi Januari 2024.
Aidha mbio za Mwenge wa Uhuru zimehitimishwa wilayani humo baada ya kukagua, kutembelea, kuweka Mawe ya Msingi kwenye Jumla ya Miradi mitano ikiwemo Barabara ya Lami yenye urefu wa Km. 0.5, Ujenzi wa Madarasa Manne pamoja na vyoo katika Shule ya Msingi Kidahwe, Kituo cha Afya Kalinzi, Kitalu cha Miche ya Kahawa kalinzi pamoja na kikundi cha wanawake ‘’Mwakeye’’ kilichopo kijiji cha Mkigo ikiwa na Thamani ya zaidi ya Shilingi Bil.1.9.
Pia mbio hizo zimezindua klabu ya kupinga Rushwa Shule ya Sekondari Bitale, Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira Shule ya Sekondari Mikamba pamoja na uzinduzi wa klabu ya Mazingira Shule ya Msingi Kidahwe na kupokea miradi yote katika Halmashauri hiyo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa