Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameuelekeza uongozi wa Serikali mkoani hapa kuwachukulia hatua watumishi watakaobainika kushiriki kuruhusu uingizaji wa mifugo wilayani Uvinza kinyume cha Sheria na kusababisha ongezeko la migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo alipozungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa wilaya ya Uvinza akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa ambapo amesema baadhi ya watumishi wa Umma wasio waadilifu wamekuwa wakipokea fedha kinyume na sharia ili kuwaruhusu wafugaji kuingiza mifugo wilayani humo bila kufuata taratibu zilizowekwa na serikali.
‘‘Mamlaka za vijiji zinapaswa kuzingatia Sheria na Kanuni za matumizi bora ya Ardhi pia nakuagiza Mkuu wa Mkoa pamoja na watendaji wako kuchukua hatua dhidi ya wale wote wanaohusika na zoezi hilo bola kuzingatia maelekezo ya serikali kuhusu taratibu za ufugaji kwani nchi haitegemei mifugo pekee’’ amesema Dkt. Mpango.
Sambamba na hayo kupitia ziara yake makamu wa Rais amekagua ujenzi wa barabara ya Malagarasi, Ilunde hadi Uvinza yenye urefu wa Km. 51.1ambayo ujenzi wake umefikia Asilimia 54 huku ikitarajiwa kukamilika Machi, 2025.
Mara baada ya kukagua mradi huo, Makamu wa Rais amemshauri Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha anatumia kipindi hiki cha kiangazi kukamilisha maeneo muhimu ya ujenzi wa barabara hiyo bila kuathiri ubora wa kazi.
Amesema lazima barabara zikamilike kwa wakati ili kutimiza malengo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu ya kutaka kuufungua mkoa wa Kigoma ili uweze kuwa Kitovu cha Biashara na Uchumi kwa ukanda wa Magharibi.
Aidha Dkt. Mpango amekagua na kuonesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa vituo vya kupoza umeme mkondo wa KV 132 kilichopo wilayani Uvinza Kata ya Nguruka wilayani Uvinza pamoja na kituo kama hico cha MV A60 kilichopo kidahwe Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Aidha Mhe. Makamu wa Rais amepata fursa ya kuzungumza na wakazi wa kijiji cha Kazuramimba na kusisitiza kuwa, serikali itaendelea kuhakikisha inasogeza huduma za jamii jirani na wananchi sambamba na kuwafuatilia kwa karibu watendaji wake ili kuimarisha kasi ya utoaji huduma.
Makamu wa Rais anaendelea na ziara yake hapo kesho Julai 9,2024 katika Manispaa ya Mji wa Kigoma kisha ataelekea wilayani Buhigwe.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa