Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ameutambulisha Mpango wa M-mama kwa Mkoa wa Kigoma wenye lengo la kupunguza vifo vya wajawazito, waliojifungua na watoto nchini kwa kuimarisha mfumo wa rufaa na usafiri wa dharura kwa bei nafuu kwa kutumia Teknolojia.
Utambulisho huo uliofuatiwa na kikao kazi umefanyika katika Ukumbi wa The Wallet Manispaa ya Kigoma/Ujiji na kuhudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Wenyeviti na wakurugenzi wa Halmashauri, wawakilishi kutoka TAMISEMI, Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Afya Mkoa, wawakilishi kutoka Vodacom Tanzania pamoja na wadau Sekta ya Afya.
Akizungumza wakati wa Kufungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa amewataka watendaji wote watakaohusika kusimamia utekelezaji wa wa Mpango huo kutanguliza weledi na uzalendo ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali yanafikiwa na kuleta matokeo chanya katika kupunguza vikwazo wanavyopitia wanawake kufikia huduma za uzazi stahiki.
Amesema iwapo wenye dhamana ya kusimamia na kutekeleza jukumu hilo watawajibika ipasavyo, jamii itaondokana na dhana ya uzazi kugeuka kuwa sababu ya vifo vya mama wajawazito, wanaojifungua pamoja na watoto wachanga kwa kuimarisha mawasiliano na uwepo wa usafiri wa uhakika katika kata zote za mkoa wa Kigoma.
‘’Tunahitaji wataalam wajengewe uwezo na jamii ijengewe uelewa kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa mpango huu, hali itakayosaidia kuondoa idadi ya vifo visivyo vya lazima vitokanavyo na tendo la uzazi kwa mama na watoto katika mkoa wetu’’
Aidha Mhe. Andengenye ametoa Rai kwa Jamii mkoani hapa kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya huduma za Jamii kujiinua na kujiimarisha kiuchumi ili kuboresha hali zao za Maisha na Maendeleo ya Mkoa wa Kigoma kwa ujumla.
‘‘Kazi nzuri za Uboreshaji na uimarishwaji wa Miundombinu zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita tuzitendendee haki kwa kuhakikisha tunaitumia miundombinu hiyo kuimarisha mifumo yetu ya kiuchumi’’ amesema Andengenye.
Akiwasilisha Taarifa ya Hali ya viashiria vya Huduma ya Afya ya Uzazi Mama na watoto kwa Mkoa wa Kigoma, Mratibu wa Huduma hiyo kimkoa Bernadetha Peter ametaja vikwazo mbalimbali vinavyosababisha mkwamo wa kufikia malengo ya uzazi stahiki kwa Mkoa wa Kigoma.
Amesema kumekuwepo na hali ya ucheleweshaji wa Rufaa kutoka vituo vya ngazi ya chini vya kutolea Huduma za Afya, ukosefu wa Elimu ya Afya na Huduma ya Uzazi miongoni mwa wanajamii pamoja na uhaba wa wataalam wenye weledi katika kutoa huduma hiyo kwa wakati.
Amezitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na uwepo wa tatizo la kifafa cha uzazi, kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua na kuchelewa kwa utolewaji wa Huduma za uzazi kwa wakati katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma hiyo.
Aidha Bernadertha ametaja idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi ambapo kwa mwaka 2018 vifo vilikuwa 78, 2029 vifo 100, 2020 vifo 119, 2021 vifo 75 na Mwaka 2022 Jumla ya vifo ilikuwa 102.
‘‘Hali ya vifo vitokanavyo na uzazi kwa mkoa wetu itapungu iwapo jamii itaupokea na kuutekeleza kwa ufanisi mfumo huu mpya wa huduma za m-mama’’ amesisitiza Bertha.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa