Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuweka mipango madhubuti kwa kushirikiana na wataalam wa Afya ili kutokomeza vifo vya Mama wajawazito mkoani Kigoma.
Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo alipotembelea na kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji akiwa katika ziara yake ya kikazi ya Siku Tatu mkoani hapa iliyolenga kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo sambamba na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
‘’Nakuagiza ndani ya kipindi cha Miezi Sita kuanzia leo Agosti 12, 2024 kutoendelea kutokea kwa vifo vya wanawake wajawazito kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika, kwani serikali imewekeza kiasi kikubwa cha Fedha kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa na kuzuia vifo vya mama wajawazito’’ amesema Mchengerwa.
Aidha Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa watoa huduma za Afya nchini kuzingatia utoaji huduma bora ikiwemo kuzingatia miiko na kanuni za utumishi wao, uadilifu na kutanguliza uzalendo katika kuihudumia jamii.
‘’Sitosita kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtumishi yeyote atakayebainika kupokea fedha kwa ajili ya kutoa huduma za Afya sambamba na kushindwa kutekeleza wajibu wake kuendana na miongozo ya utumishi wake’’ amesisitiza Waziri Mchengerwa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri amemuelekeza Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe OR TAMISEMI kufuatilia Fedha serikali kiasi cha Shilingi Bil.2 kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo 16 katika Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Sambamba na agizo hilo Mchengerwa amemuelekeza Mkurugenzi huyo kufuatilia ili serikali iweze kutoa kiasi cha Shilingi Mil. 300 kwa ajili ya kukamilisha kituo cha Afya Kagunga kilichopo Halmashauri ya wilaya ya Kigoma na kukiwezesha kutoa huduma ili kuwaondolea wananchi adha ya kufuata huduma za matibabu nchi jirani ya Burundi.
Kupitia ziara hiyo, Mhe. Mchengerwa ametoa pongezi kwa Wakala wa Barabara vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuyaunganisha maeneo mbalimbali ya mkoa kupitia ujenzi wa madaraja ya mawe ambayo ujenzi wake hutumia gharama nafuu na kuipunguzi mzigo serikali.
Akikagua ujenzi wa barabara ya Ujiji Bangwe kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa Km.7 inayotekelezwa chini ya mradi wa TACTICS, Mhe Mchengerwa ameonesha kutoridhishwa na mkandarasi anayetekeleza mradi huo kutokana na kuwa nyuma katika utekelezaji wa mradi tofauti kwa Asilimia 18 badala ya 60 ya mkataba wake ambapo amesisitiza kuwa serikali itafuatilia ili kuwabaini wakandarasi wote wanaochelewesha miradi ili wasipewe tena kazi za miradi kama hiyo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa