Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba ameishukuru Serikali kwa kuwezesha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoa fursa ya upatikanaji wa Klinikiya Matibabu ya Himofilia na Selimundu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma-Maweni.
Akimuwakilisha Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya Prof. Paschal Rugajo katika Hafla ya Uzinduzi wa Kliniki hiyo, Dkt. Leba amesema kuanza kutolewa kwa matibabu hayo mkoani hapa kutarahisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa gharama nafuu na ukaribu kwa wagonjwa katika Kanda ya Magharibi.
Amesema hapo awali wagonjwa walilazimika kutumia muda mrefu na Gharama kubwa kuifikia huduma hiyo, tofauti na sasa ambapo huduma itatolewa kwa ukaribu zaidi kwa wagonjwa katika Mkoa wa Kigoma na ile ya jirani.
‘‘Kusogezwa kwa huduma hii kutasaidia wananchi kupatiwa elimu ya ugonjwa wa Himofilia, kupimwa kwa wakati ili kubaini aina ya Himofilia inayomsumbua mgonjwa na kutibiwa kwa muda sahihi, hali itakayo punguza Madhara ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza’’ amesema Dkt. Leba.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Maweni Dkt. Stanley Binagi amesema Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kushirikiana na wadau wake wenye lengo la kukabiliana na kutokomeza Ugonjwa wa Himofilia na Selimundu, wamewezesha kufanyika kwa maboresho katika Jengo Maalum la Kliniki, upatikanaji wa vifaa Tiba pamoja na Matibabu ya ugonjwa huo.
Binagi amesisitiza kuwa, matibabu ya ugonjwa huo yatatolewa bure hivyo wenye changamoto hiyo wasisite kufika Hospitalini hapo huku akiwashukuru (MNH) pamoja na wadau wake kwa kutoa mafunzo kwa matabibu katika Hospitali ya Mkoa, wilaya na vituo vya Afya vya Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalam hao katika kuwatambua wagonjwa, kutoa Matibabu pamoja na ushauri kwa wagonjwa wa Himofilia
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa