Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Mhe. Hassan Rugwa amesema uwepo wa Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Kigoma umechangia kuisaidia serikali kwa kiasi kikubwa katika kutatua changamoto za wananchi kupitia utekelezaji wa afua mbalimbali kwa lengo la kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Mhe. Rugwa ametoa kauli hiyo alipofungua Mkutano wa Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Kigoma uliolenga kupitia taarifa za utendaji kazi wa Mashirika hayo kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2023 na kusisitiza kuwa wadau hao wamekuwa mchango mkubwa kupitia afua mbalimbali wanazotekeleza ikiwemo kwenye sekta ya toaji wa huduma za jamii, Maendeleo ya Jamii, utawala bora, sambamba na utunzaji wa Mazingira.
Kupitia hotuba yake, kiongozi huyo amezitaja changamoto mbalimbali zinazoyahusu mashirika hayo kuwa ni pamoja na kutegemea zaidi wafadhili katika utekelezaji wa majukumu yao hivyo ufadhili unapokoma au kulegalega husababisha ufanisi wa mashirika hayo kuwa mdogo au kushindwa kabisa kujiendesha na kusababisha baadhi ya mipango kutokamilika.
‘’Hali hii huchangia kwa kiasi kikubwa mashirika mengi kutekeleza majukumu kwa kuzingatia matakwa ya wafadhili badala ya kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi katika mazingira waliyopo’’amesema Rugwa.
Ameitaja changamoto nyingine kuwa ni mashirika mengi kutekeleza majukumu yao katika maeneo ya mijini badala ya kujielekeza vijijini ambapo pia kuna mahitaji makubwa ya kijamii.
‘’Niwasisitize kuzingatia na kujielekeza maeneno yote ya mijini na vijijini mnapoweka mipango ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili wanakigoma wote waweze kunufaika na utendaji kazi wenu’’ amesema Rugwa.
Rugwa ameyataka mashirika hayo kutoa taarifa za utekelezaji wa kazi zao kwa wananchi katika maeneo wanayotoa huduma ili wakazi waweze kufahamu maendeleo na matokeo ya kazi hizo wanazozifanya.
Aidha kupitia hotuba yake, Katibu Tawala ameyataka Mashirika hayo kujenga utamaduni wa kufanya utafiti utakaoshirikisha wananchi ili waweze kutoa maoni kuhusu mahitaji yao ili huduma zinazotolewa na mashirika hayo ziweze kuwagusa moja kwa moja.
Utakuta kuna maeneo yanamashirika zaidi ya moja na kazi wanazofanya zinafanana, hivyo niwatake mkafanye utafiti na kutawanya huduma zenu katika maeneo yote ya mkoa badala ya kujikita mijini au katika halmashauri chache huku maeneo mengine yakikosa huduma.Aidha katibu tawala huyo ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mashirika hayo ili yaweze kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Kigoma wanapata huduma muhimu.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255738192977
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa