Vijana mkoani Kigoma wametakiwa kujitokeza na kushiriki Mashindano ya mchezo wa soka ya Ujirani Mwema yanayohusisha Nchi za Tanzania na Burundi ili waweze kupata fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kufungua milango ya ajira kupitia Tasnia hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa mashindano ya mchezo wa Soka ya Ujirani Mwema ambaye pia ni Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Kigoma Revocatus Lutera, ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa mashindano hayo yatakayozihusisha Timu kutoka katika wilaya za Mkoa wa Kigoma pamoja na Mikoa ya Burundi inayopakana na Tanzania.
‘’Vijana wajitokeze wakati wa mchakato wa uundaji wa Timu hizi zinazoandaliwa kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Ujirani mwema, hii itawapa fursa ya kutambulisha vipaji vyao na kujiweka katika Soko la mchezo huo maarufu kwa uzalishaji wa ajira ndani na nje ya nchi’’amesema.
Katika mashindano hayo, Mkoa wa Kigoma utawakilishwa na timu za Muungano kutoka Halamashauri za Kakonko na Kibondo, Kasulu na Buhigwe, Kasulu Mji na Uvinza pamoja na Halmashauri ya Mji na wilaya Kigoma.
‘‘Mashindano yanatarajiwa kufanyika katika Mkoa wa Makamba nchini Burundi kuanzia Novemba 14, 2022 hadi 19, 2022 yakihusisha timu nane ambapo nne ni kutoka Tanzania mkoani Kigoma na nne kutoka Burundi na mpaka sasa maandalizi yamekamilika’’ amesema Lutera.
Michezo hiyo imekuwa ni muendelezo wa utamaduni wa Ujirani mwema na kuunganisha jamii za wakazi jirani wa nchi hizi mbili kwa kuwakutanisha kila mwaka kupitia mchezo huo pendwa Duniani, ambapo zawadi za washindi hutolewa na mdhamini mkuu wa Mashindano ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Tawala nchini Burundi (CNDD-FDD) Revelian Ndikuriyo.
Aidha, mashindano hayo yaliyoanzishwa Julai 29, 2017 kupitia kikao cha Ujirani Mwema cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma na Mikoa ya Burundi inayopakana na Kigoma, yanalenga kudumisha ulinzi na Usalama, kukuza urafiki, ushirikiano, upendo na undugu baina ya nchi hizi mbili.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa