Wakazi mkoani Kigoma wametakiwa kuyatumia Maonesho ya Mfuko na Program za uwezeshaji kujifunza namna ya kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Mkoa kwa ajili ya kujiinua, kujiendeleza na kujiimarisha kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli alipotoa Taarifa kwa Umma kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuhusu uwepo wa Maonesho ya Sita ya Mfuko wa Uwezeshaji Kitaifa Mkoani hapa yanayotarajia kufunguliwa Mei 23, 2023 na Naibu Waziri wa Viwanda, Uwekezaji na Biashara Mhe Exaud Kigahe.
Amesema Mkoa umepata bahati kuwa kitovu cha Maonesho hayo muhimu hivyo wakazi waitumie fursa hiyo adhimu kwa ajili ya kupata uwezeshwaji wa kitaalam na kiuchumi ili kujiendeleza na kujiimarisha kiuchumi kupitia Nyanja za Biashara na uwekezaji.
‘‘Nitoe wito kwa wa kazi wa Mkoa wa Kigoma kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kupata maarifa mapya kuhusiana na taratibu mbalimbali za kuwezeshwa na kujiimarisha kiuchumi kupitia fursa zilizopo ndani na nje ya mkoa kwa lengo la kujiletea Maendeleo’’ ameeleza Kalli.
Naye Linda Mshana ambaye ni Meneja Masoko na Uwezeshaji kutoka Mfuko wa Self, amesema maonesho hayo yanatoa fursa ya kutoa huduma na mafunzo wezeshi ya kiuchumi kupitia mifuko ya Serikali ya Program za uwezeshaji wananchi kiuchumi, Taasisi wezeshi katika uanzishaji na uendelezaji wa Biashara pamoja zile zinazotoa huduma kwa Jamii.
Amesema Pamoja na kuendesha mafunzo, zitatolewa huduma za mikopo kwa wananchi watakaokidhi vigezo kwa lengo la kuanzisha na kuendeleza shughuli za Kilimo na ufugaji, kuanzisha na kukuza Biashara pamoja na kuboresha uzalishaji kwa wenye viwanda vidogo na vya kati.
Maonesho hayo yaliyoanza Mei 21, 2023 katika Uwanja wa Mwanga Community Centre, Manispaa ya Kigoma/Ujiji yanatarajiwa kufungwa Mei 27, 2023 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa