Makatibu wakuu wanne wa wizara na wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ardhi, Maendeleo ya Mifugo wamekutana mjini Kigoma kusaka suluhu ya uvamizi unaofanywa kwenye hifadhi za misitu na mapori ya akiba katika maeneo mbalimbali nchini, tatizo ambalo limekuwa likiitesa Serikali.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda ambaye ndiye Mwenyekiti wa kikao hicho, anakiri kuwapo uvamizi wa misitu wa aina tofauti unaofanywa katika namna mbalimbali, ikiwamo kuanzisha makazi na kusajili ama vijiji au vitongoji katika misitu ya hifadhi mkoani Kigoma.
Anasema, ni hali inayochangia uwepo wa uharibifu wa misitu kutoka kwa wanavijiji na wageni wanaoingia kutoka nchi jirani katika vijiji hivyo.
Profesa Mkenda anasema ufugaji holela wa mifugo ikiwamo kilimo na ufugaji holela wa kuhamahama, vijiji vingi kukosa mipango ya matumizi bora ya ardhi ni jambo jingine linalochochea uharibifu wa hifadhi za misitu.
Sababu nyingine anayotaja kuchangia uharibifu katika hifadhi za misitu nchini, ni pamoja na kuwapo mgawanyiko wa usimamizi kati ya serikali kuu na serikali za mitaa.
“Sekta ya misitu inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kugawanywa kwa usimamizi wa hifadhi hizo kati ya serikali kuu na serikali za mitaa, jambo linaloleta mwingiliano wa kazi na kupishana kwa vipaumbele vya uhifadhi. Hata suala la ufugaji Mkoa wa Kigoma ni tishio Zaidi kwa ustawi wa misitu,” anasema Profesa Mkenda.
Anafafanua kwa kusema ufugaji ndani ya misitu mkoani Kigoma unafanywa na wenyeji na watu kutoka nchi jirani wakifanya kazi hiyo kwa kushirikiana.
Profesa Mkenda anasema kutokana na chanagmoto hizo Serikali imeamua kuchukua hatua za kuhakikisha wanakomesha vitendo hivyo kwa nguvu zote kwa kukutanisha makatibu wakuu wa Wizara zote zinazohusika.
Anasema kazi yao nikutoa mapendekezo kwa mawaziri wa wizara husika juu ya namna bora ya kumaliza tatizo la wafugaji kuvamia misitu kwa kuzingatia masilahi mapana ya taifa. Ripoti ambayo wataikabidhi Januari 04, 2018.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel, amekiri kutambua tatizo la wafugaji kuvamia hifadhi za misitu na kuwataka wafugaji hao kujiandaa na kutii maamuzi yatakayotolewa na Serikali.
Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo anataja mbinu zinazotumika kudhibiti uhariubifu wa misitu kuwa ni ulinmzi shirikishi ambapo TFS hushirikiana na wanachi kupambana na hali hiyo, matumizi ya intelijensia kuzuia uhalifu, pamoja kuimarisha ushirikiano wa kikanda na nchi jirani.
Makatibu Wakuu wengine waliohudhuria kikao hicho ni Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Tixon Nzunda na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mathias Kabunduguru.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255738192977
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa