Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango ametembelea na kukagua maendeleo ya Miradi ya Elimu na Afya inayotekelezwa katika Kijiji cha Kasumo wilaya ya Buhigwe Mkoani hapa.
Mh. Mpango amekagua ujenzi wa shule ya Sekondari ya wasichana Kidato cha Tano na Sita yenye jumla ya Majengo 18 yanayojengwa kwa Thamani ya Shilingi Bilioni Moja katika kijiji hicho na kuridhishwa na kazi zinazoendelea kufanywa na mafundi pamoja na wasimamizi wa mradi huo.
Aidha, amekagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kasumo unaotekelezwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Serikali wenye thamani ya Shilingi Milioni 133 ambao unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba 2022.
Baada ya kukagua miradi hiyo, Makamu wa Rais amewapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kujitolea kutekeleza mradi wa Zahanati, huku akisisitiza wanafunzi watumie fursa ya uwepo wa miundombinu ya kielimu inayoendelea kujengwa ili kujiendeleza kitaaluma na kupata wataalamu mbalimbali kwa manufaa ya Taifa.
Amewaagiza wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa shule kupanda miti pembezoni mwa majengo ili kupendezesha na kulinda mazingira pamoja na kupunguza Athari zinazoweza kusababishwa na upepo mkali.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amechangia jumla ya mifuko 200 ya Saruji pamoja na kuendesha harambee iliyofanikisha kupatikana kwa mifuko 410 iliyokuwa inahitajika ili kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kasumo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa