Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amesema Serikali itanedelea kuhamasisha na kusimamia kilimo cha mazao ya kimkakati nchini ikiwemo zao la chikichi ili kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Waziri Majaliwa ametoa kauli hiyo alipoongoza kikao kazi kilichowawakutanisha wadau wa zao la Chikichi Mkoani Kigoma, kilicholenga kufanya Tathimini ya mafanikio pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha kilimo cha zao hilo.
Amesema Serikali imeamua kuongeza nguvu katika uwekezaji wa Kilimo cha chikichi kwa lengo la kuhakikisha kunakuwepo na utoshelevu katika upatikanaji wa mafuta ya kula nchini ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kuagiza huduma hiyo muhimu nje ya nchi.
‘‘Viongozi wa Serikali hakikisheni mnawaelimisha wananchi, kuwasaidia kupata miche na kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kilimo cha zao la chikichi katika maeneo yenu ili waweze waweze kujiinua kiuchumi na kuongeza upatikanaji wa huduma ya mafuta ya kula yanayotengenezwa ndani ya nchi’’ Amesema Majaliwa.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuimarisha vituo vya utafiti wa mbegu bora za Chikichi ndani na nje ya Mkoa wa Kigoma, kwa lengo la kuongeza uzalishaji utakaowaletea tija wananchi.
Aidha Majaliwa amesisitiza taasisi za kifedha kuendelea kutoa mikopo kwa Wananchi wanaojishughulisha na kilimo cha zao hilo pale watakapothibitika kukizi vigezo vya kupata mikopo hiyo.
Akiwasilisha Taarifa ya hali ya uzalishaji na usambazaji wa chikichi aina ya TENERA nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) Mhandisi Geofrey Mkamilo amesema hadi kufikia Februari 2023, miche 621,213 yenye Thamani ya Shilingi Bil 1.7 imegawiwa bure ndani na nje ya Mkoa wa Kigoma kwa lengo la kuimarisha kilimo cha zao hilo la kimkakati.
Amefafanua kuwa, katika upandaji wa zao la chikichi, Mkoa wa Kigoma ni wapili kitaifa ambapo wakazi wamefanikiwa kupanda miche 58,445 ambayo imepandwa katika Ekari 1,124 huku Halmashauri ya wilaya na Mji Kasulu ikiongoza kwa wananchi kupanda miche bora 42,582 katika eneo lenye ukubwa wa Jumla ya Ekari 819.
Upande wao wadau kutoka Taasisi za kifedha mkoani Kigoma waliopata fursa ya kushiriki kikao hicho, wamesema wanaendelea kutoa mikopo kwa wakulima wa zao la chikichi ili kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea kupitia kilimo na uchakataji wa zao la chikichi.
Aidha wameiomba Serikali kuweka utaratibu mzuri kwa ajili ya kutatua changamoto mchakato wa masherti na vigezo vya Dhamana baina ya wakulima na Taasisi hizo ili kurahisisha zoezi la utoaji wa Mikopo kwa wakulima.
Baadhi ya wadau wa Kilimo cha zao la chikichi waliojitokeza na kushiriki kikao kazi hicho wamemshukuru Waziri Mkuu kwa kujikita katika kuhamasisha na kusimamia kilimo cha zao hilo mkoani Kigoma na kusisitiza kuwa, wameanza kuona faida zake kiuchumi na ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa