Madaktari bingwa wa Dkt. Samia wameanza Kambi maalum ya Matibabu ya Kibingwa mkoani Kigoma ambapo wataanza kutoa Huduma za kiafya kwa Siku Sita kuanzia leo Oktoba 7, 2024 katika Hospitali Nane (8) za Halmashauri za Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza mara baada ya kuwapokea madaktari hao, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa ya uwepo wa madaktari hao kwa lengo la kupata matibabu ya kibingwa jirani na maeneo yao badala ya kuyafuata katika Hospitali za mbali hivyo kuokoa muda na gharama kubwa pamoja na usumbufu wa kusafirisha wagonjwa wao.
Mhe. Rugwa amewataka madaktari hao kubaini changamoto za kimatibabu zilizopo mkoani Kigoma na kutoa ushauri namna bora ya kuzikabili ili kuimarisha utoaji wa huduma mkoani Kigoma kupitia maboresho ya sera za huduma za Afya.
‘’Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa inayopakana nan chi jirani hivyo mnapoenda kutoa huduma muutumie muda huo kubaini maradhi ambayo hayapo maeneo mengine ya nchi ili kwa pamoja tuweze kuyadhibiti yasiweze kusambaa katika mikoa mingine’’amesema Rugwa.
Aidha Katibu Tawala ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kusogeza huduma mbalimbali ikiwemo huduma za Afya kwa wakazi mkoani Kigoma na Tanzania kwa ujumla na kuwarahisishia wananchi utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazohusu afya zao.
Jackline Ndanshau Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya amesema kambi hiyo ya Madaktari wa Samia itafanyika kwa muda wa siku sita kuanzia Oktoba 7 hadi 12,2024 na itahusisha Hospitali zote za Halmashauri ambapo kila kituo kitapokea madaktari saba (7) ikiwa ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, watoto na watoto wachanga, usingizi na ganzi, magonjwa ya ndani, upasuaji na mfumo wa mkojo pamoja na muuguzi bingwa.
Amefafanua kuwa upande wa Hospitali za Halmashauri za Mjini(karibu na Hospitali za Rufaa na za Mkoa) watapokea pia daktari bingwa wa mifupa hivyo maeneo hayo timu itakuwa na jumla ya wataalam nane(8).
Ndanshau ameeleza kuwa lengo la serikali ni kusogeza huduma bobezi na zile za kibingwa katika Halmashauri zote 184 nchini, kuimarisha ujuzi wa wataalam wa Afya waliopo kazini sambamba na kuimarisha na kuanzisha wodi maalum za watoto wachanga wagonjwa na waliozaliwa na uzito pungufu.
PICHA ZA PAMOJA.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa