Maboresho ya Mifumo Serikalini Kuongeza Uwajibikaji
Posted on: August 13th, 2017
Maboresho katika Mifumo ya Sekta za umma yametajwa kuwa Kichocheo cha Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa yatasaidia kutoa mrejesho wa mara kwa mara kwa ngazi zote za Utawala kwa wakati.
Akizungumza wakati akifungua Mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo kutoka Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, Muwakilishi wa Katibu tawala wa Mkoa wa Kigoma Bw. Samwel Tenga ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema dhamira ya Serikali ni kuona watoa huduma wanaweza kujipima kwa kuangalia matokeo kwa kuwa mfumo huu ulioboreshwa utaongeza uwazi,ufanisi na uwajibikaji katika utoaji huduma kwenye sekta za umma.
“Kutokana na maboresho na kurahisishwa kwa Teknolojia,mfumo huu mpya wa PlanRep umefanywa kuwa ‘web based’ hivyo utawezesha Halmashuri kuingiza taarifa za Mipango na Bajeti moja kwa moja kwa njia ya mtandao na kuweza kutumwa kwenye mfumo mmoja uliopo Ofisi ya Rais TAMISEMI na hatimaye kuingizwa kwenye bajeti kuu ya mwaka husika,” Alieleza Tenga.
Akifafanua Bw. Tenga amesema kuwa utaratibu wa awali wa kuandaa bajeti na Mipango ulitumia rasilimali nyingi ikiwemo fedha na muda hali iliyozorotesha utoaji wa huduma ambapo kwa sasa changamoto hizo zitaondolewa na mfumo mpya ulioboreshwa.
Ameeleza kuwa mfumo utasaidia kuongeza tija na kuwawezesha watumishi katika maeneo ya kutolea huduma kuwa na muda wa ziada katika kuwahudumia wananchi kwa kuwa mipango na bajeti vitafanyika katika vituo vya kutolea huduma.
Aliongeza kuwa Halmashuri sasa zitatakiwa kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi kwa kuwa PS3 imekuwa katika zoezi la kufunga mitambo ya intaneti Local area network-LAN katika Halmashuri 93 zilizopo katika mradi hivyo alizitaka Halmashauri zote kuhakikisha kuwa zinatumia vyanzo vyake vya mapato kuweka LAN ili kuongeza kasi yakuwahudumia wananchi.
Pia alipongeza PS3 kwa kuandaa mafunzo yakuwajengea uwezo watumiaji wa mfumo huo,Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa Maboresho ya Sekta za Umma kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani USAID ambao wamekuwa washirika wa maendeleo wa Serikali kwa muda mrefu hali iliyopelekea kuwepo kwa mafanikio makubwa siku hadi siku katika Mikoa na halmashuri hapa nchini.
Akizungumzia faida za mfumo huo amesema kuwa utasaidia Serikali kuokoa rasilamli fedha zilizokuwa zikitumika awali kuandaa bajeti na mipango yake kuanzia ngazi ya watoa huduma hadi Taifa hivyo matokeo ya kuwepo kwa mfumo wa PlanRep ulioboreshwa yataonekana kupitia huduma wanazopata wananchi mara utakapoanza kutumika mwaka wa fedha 2018/2019.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi wa PS3 Dkt. Emmanuel Malangalila amesema Dhamira ya mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ni kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mifumo hiyo ili kuongeza tija na kuboresha huduma za Serikali kwa jamii hasa zile zenye uhitaji zaidi.
Akifafanua Dkt. Malangalila amesema mradi huo utatekelezwa kwa miaka mitano na utakamilika ifikapo mwaka 2020, Mfumo huo utatumika kuleta uwiano kati ya matumizi na huduma zitolewazo.
Aliongeza kuwa mafunzo ya PlanRep yanawashiriksha washiriki takribani 92 kutoka Halmashuri 16 za mikoa ya Kigoma,Rukwa na Katavi.
Naye muwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI bw. Elisa Rwamiago akizungumza wakati wa mafunzo hayo amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuleta mabadiliko katika mifumo ya kiutendaji Serikalini hasa katika swala zima la Kupanga Bajeti,Mipango na Kutoa ripoti hali itakayosaidia kufikiwa kwa maendeleo ya kweli kwa wananchi kupitia huduma na miradi inayotekelezwa katika maeneo yao kwa kuzingatia vipaumbele vyao.
Mradi wa PS3 unalenga kushirikiana na Serikali katika kuboresha matumizi ya rasilimali zilizopo ikiwemo fedha na rasilimali watu katika ngazi ya kutolea huduma kama vile vituo vya Afya,Zahanati,Hosipitali na katika sekta ya elimu.