MKUU WA MKOA WA KIGOMA THOBIAS ANDENGENYE (KULIA) AKIKAGUA MAENDELEO YA UTEKELEZAJI WA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA KIELIMU KATIKA HALMASHAURI YA MJI KASULU.MKUU WA MKOA WA KIGOMA THOBIAS ANDENGENYE AKISHIRIKI KAZI YA UCHANGANYAJI WA ZEGE ALIPOKUWA KATIKA ZIARA YA KUKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA KIELIMU KATIKA HALMASHAURI YA MJI WA KASULU. KULIA KWAKE NI WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU) PROF. JOYCE NDALICHAKO MBUNGE WA JIMBO LA KASULU MJINI.
Ujenzi wa Miundombinu ya Elimu karibu na makazi ya wananchi utapunguza matukio ya unyanyasaji pamoja na ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike wanaosoma ngazi ya Elimu Msingi na Sekondari ikiwemo kupungua kwa vitendo vya ubakaji, mimba na ndoa za utotoni hali inayosababisha kundi hilo kutofikia malengo ya kielimu.
Changamoto hizo zimekuwa zikisababishwa na wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kielimu, hali inayosababisha baadhi ya watoto wa kike kurubuniwa na watu wasio waadilifu kwa kuwapa misaada midogo ikiwemo fedha na usafiri kisha kutekeleza adhma zao.
Baadhi ya vijana wanaosafirisha abiria kwa kutumia usafiri wa pikipiki (bodaboda) wametajwa kuhusika kuwarubuni mabinti kwa kuwapa msaada wa usafiri au kutumia fursa ya upweke wakiwa safarini kuwashawishi au kuwalazimisha kufanya vitendo vya ngono wakiwa katika maeneo ya mapori.
Hili ni jambo baya linalotweza utu wa mtoto wa kike, kuhatarisha usalama wa Afya zao pamoja na kukatisha ndoto zao kutokana na kupata maradhi, ujauzito au kujiingiza katika ndoa za utotoni.
Pamoja na hayo, uwepo wa wenye nyuma ambao huwapangisha wanafunzi wa kike na kuwarubuni kwa kuwawezesha mahitaji mbalimbali kama chakula, mavazi, vipodozi hata kusamehe gharama za pango ili kufanikisha tamaa zao za kimwili nayo ni changamoto dhidi ya kundi hilo.
Sambamba na hilo baadhi yao hutoka nyumbani bila kupata kifungua kinywa kutokana na baadhi ya familia kushindwa kuweka utaratibu wa kuwapa watoto chakula asubuhi huku wakitembea umbali hadi Km. 20 kwenda na kurudi shuleni. Hali hii hutengeneza mazingira ya mabinti kukubali kupokea fedha kwa watu wasio waadilifu ili waweze kumudu kununua vyakula shuleni nyakati za mapumziko.
Mkoani Kigoma imejengeka tabia ya masoko ya usiku na imeendelea kuwa dimba huru la makutano ya vijana na mabinti hali inayotoa mianya kwa wale wanaoishi mbali na wazazi wao hususani wanaopanga kwa ajili ya kufuata huduma za kielimu, kujikuta wapo huru na kuutumia muda huo kuingia ushawishi na k ujikuta wakishiriki vitendo visivyo vya kimaadili.
Hili huenda sambamba na baadhi ya wazazi kuwatumia watoto wa kike kwa shughuli za kibiashara ikiwemo kupeleka mazao mbalimbali pamoja na bidhaa nyingine kwenye masoko ya jioni ili kuipatia Familia kipato kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali.
Kadhalika baadhi ya njia za kuelekea shuleni huwalazimu kupita katika mapori, mashamba au nyakati nyingine wanafunzi hujikuta wakirejea nyumbani usiku kutokana na kucheleweshwa na mvua kali au uwepo wa majukumu mbalimbali ya shuleni, jambo linaloweza toa mwanya kwa watu wasio waadilifu kutumia mazingira hayo kufanya vitendo vya kikatili dhidi ya kundi hilo.
Afisa Elimu wilaya ya Kibondo Bi. Oliver Mgeni anasema kukamilika kwa shule ya Msingi Mahaha kutawapunguzia adha wanafunzi wanaotoka katika Kitongoji cha Mahaha katika kijiji cha Magalama wilayani humo kutembea umbali wa hadi Km. 20 kwa ajili ya kufuata huduma ya Elimu katika Shule ya Msingi iliyopo katika kijiji jirani cha Magalama wilayani humo.
Huo ni moja wapo ya mfano wa wa adha walizokuwa wakikabiliana nazo watoto wetu kwa kutembea umbali mrefu katika mazingira yenye jua, mvua huku baadhi yao wakienda umbali huo bila kuweka chochote tumboni.
Serikali kupitia mradi wa Mpango wa kuboresha Elimu ya Msingi (BOOST) na pamoja na Mpango wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) imeendelea kumarisha miundombinu ya kielimu katika shule za Msingi na Sekondari mkoani Kigoma jambo ambalo kwa Asilimia kubwa litapunguza au kuondoa kabisa adha hizo na kutoa fursa kwa kundi hilo kuzifikia ndoto zao kupitia Elimu.
Kupitia mradi wa BOOST serikali mkoani hapa imefanikiwa kujenga vyumba vya Madarasa 159 katika shule kongwe pamoja na ujenzi wa shule mpya za msingi 16 ikiwa ni shule mbili kwa kila halmashauri. Aidha kupitia mpango wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), serikali imejenga jumla ya shule 17 katika Halmashauri zota nane za mkoa hususani katika kata ambazo hazikuwa na shule za Sekondari.
Hakika hili ni suala la kupongwezwa na pongezi hizi ziwafikie wadau wote wa Elimu kwa ngazi zote mkoani Kigoma kwa kufanikiwa kutumia miradi hiyo kuendelea kuwanusuru watoto wetu dhidi ya adha hizo ambazo pamoja na kuwaathiri kwa kiasi kikubwa watoto wa kike athari hizo zinaigusa jamii kwa ujumla.
Mfano suala la kutembea umbali mrefu, kushinda bila kupata chakula pamoja na adha za mvua na jua kali, athari zake ni kwa watoto wote bila kutofautisha wa kiume au wa kike.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye kupitia mikutano yake na wananchi amekuwa akiwakumbusha majukumu matatu ya msingi ikiwemo kutunza familia, kuhakikisha watoto wanakula shuleni pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali katika katika kuboresha miundombinu ya kielimu.
Waswahili wanasema mtoto wa Mwenzio ni wa kwako, wakati serikali inaendelea kuyagusa mazingira yenye changamoto hizo kwa watoto wetu, jamii inapaswa kudumisha ulinzi kwa watoto dhidi ya unyanyasaji na vitendo vingine vya ukatili pamoja na kujitolea kufanya kazi mbalimbali zinazohusu utekelezaji miradi ya Maendeleo pale inapohitajika kufanya hivyo.
Pongezi za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ya kupelekeka fedha nyingi kwenye miradi ya Elimu mkoani Kigoma.
Ni jambo la kutia moyo katika karne hii kuona mtoto aliyepo kijijini anasoma kwenye darasa lenye miundombinu ya Umeme, madirisha yenye vioo pamoja na kila mtoto kukaa kwenye kiti na meza yake huku wakitumia vyoo bora na vya kisasa.
Jukumu letu wazazi na walezi ni kuendelea kuwabiidisha watoto wetu ili waweze kujisomea, kufuatilia maendeleo yao darasani pamoja na kuwapunguzia majukumu ili wapate muda wa kutosha kwa ajili ya kujisomea na kupumzika wawapo nyumbani.
Aidha Wito wa kuchangia chakula ili watoto waweze kula shuleni ni jambo muhimu sana kwani sambamba na kuwapa utulivu watoto wakiwa darasani, litatupunguzia changamoto ya udumavu na utapiamlo jambo ambalo ni hatari sana kwa afya ya Akili ya mtoto.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa