Wajumbe wa Mabaraza ya Kata Mkoani Kigoma wametakiwa kutekeleza majukumu yao ya kisheria kwa kujikita katika kusuluhisha mashauri mbalimbali yanayojitokeza katika Jamii zao huku wakijiepusha na jukumu la kutoa hukumu juu ya mashauri hayo kwani kufanya hivyo ni kuingilia majukumu ya kimahakama.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Kigoma, Msafiri Nzunuri alipokuwa akizungumzia kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria yanayotarajiwa kufanyika kimkoa wilayani Kibondo.
Amesema baadhi ya wajumbe kwa kushirikiana na watendaji hujikuta wakikiuka sheria na mipaka ya utendaji kazi wao kwa kutoa hukumu za mashauri wanayopelekewa na wananchi katika maeneo yao, huku wakijua wazi kuwa jukumu hilo kisheria linatekelezwa na ngazi mbalimbali za kimahakama.
‘‘Hukumu yoyote inapotolewa kisheria huzingatia vifungu vya Sheria, utoshelevu wa ushahidi kutoka pande zote mbili pamoja na kusimamiwa na watu wenye weledi kwa kuwa na Taaluma ya Sheria’’ amesema.
Amesisitiza kuwa, jukumu la msingi la mabaraza ya kata kiusuluhishi kwa kushirikiana na watendaji wa kata ni kulinda amani na utulivu kwa kuwasaidia wahusika wa migogoro kufikia muafaka katika ngazi ya kata husika. Aidha migogoro hiyoisuluhishwe kwa njia za kirafiki pande zote zote mbili za mgogoro.
Kuhusu Maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria, Msafiri amesema utungaji wa Sheria Namba 1 ya Mwaka 2017 unalenga kuongeza upatikanaji wa Haki kwa wote huku ukiwajumuisha watu wenye uwezo duni wa kupata huduma za kisheria kwa mawakili kutokana na kushindwa kumudu gharama.
Amefafanua kuwa, Maadhimisho hayo yamelenga kuongeza uelewa wa kisheria kwa jamii juu ya haki za watoto, wanawake na makundi mengine yanayolengwa kwa lengo la kukomesha unyanyasaji wa kijinsia na ukatili nchini kote kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria.
Maadhimisho ya wiki ya msaada kisheria yanafanyika kwa wiki moja kuanzia tarehe 5 hadi 10 Desemba 2022 nchini kote yakilenga kutoa elimu ya kisheria, kupokea na kutatua malalamiko ya kisheria, kubainisha maeneo ya huduma za kisheria, kuendesha kampeni za hamasa kwa Umma kuhusu umuhimu wa kutumia msaada wakisheria pamoja na kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa watu walioko maeneo ya vizuizi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa