Wafanyabiashara mkoani Kigoma wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa mabaraza ya Biashara kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuibua fursa mpya za kiabiashara badala ya kutumika kwa ajili ya kutatua migogoro ya wafanyabiashara pekee.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye alipozungumza wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Biashara Mkoa wa Kigoma uliofanyika katika Hoteli ya Lake Tanganyika iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha Mazingira ya uwekezaji mkoani Kigoma ili kutimiza dhamira ya Mhe. Rais ya Dkt. Samia Suluhu ya kuufanya mkoa kuwa kitovu cha Biashara kwa ukanda wa Magharibi.
Amesema ili kuleta tija kibiashara mikutano ya mabaraza ya biashara isitumike kutatua changamoto za wafanyabiashara pekee bali iweke mikakati ya pamoja katika kuibua fursa za kibiashara na uwekezaji ili kuinua uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
‘’Iwapo mikutano hii itafanyika mara kwa mara, itaondoa migogoro isiyo ya lazima na kutuepusha migomo ya wafanyabiashara inayoweza kujitokeza kutokana na changamoto zilizopo kupata utatuzi kwa wakati hii’’ amesema Andengenye.
Amesema Serikali imeelekeza zaidi ya Shilingi Tri. 8 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji mkoani Kigoma sambamba na kufanya ukarabati wa meli za Mt. Sangara, MV Liemba pmaoja na Mwongozo kwa ajili ya kujenga mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya mkoa wa Kigoma kusafiri wao wenyewe na kusafirisha bidhaa zao.
‘‘Serikali ya awamu ya Sita inaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika wa Gridi ya Taifa , kuboresha uwanja wa ndege pamoja na ujenzi wa barabara zinazouunganisha mkoa na mikoa ya jirani kwa kiwango cha Lami’’ amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesema Serikali itaendelea kupokea na kufanyia kazi maoni ya wafanyabiashara pamoja na kutatua changamoto zao kwa haraka ili kuwawekea mazingira rafiki wafanyabashara na kuwawezesha kufikia malengo waliyojiwekea.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa