Balozi mdogo katika ubalozi wa Burundi mkoani hapa Kekenwa Jeremie amekabidhi Mipira Mia moja kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ikiwa ni sehemu ya Maandalizi ya Mashindano ya Ligi ya Ujirani Mwema(Tanganyika Cup) kwa Timu za Vijana chini ya Miaka 18 kwa Mwaka 2023.
Mipira hiyo ni utangulizi wa mipira 150 iliyoahidiwa kutolewa na Katibu Mkuu wa Chama Tawala nchini Burundi CNDD-FDD Reverian Ndikuriyo kwa ajili ya Maandalizi ya ligi ya Tanganyika Cup pamoja na Dhamira yake ya dhati katika kuibua na kukuza vipaji vya Soka kwa Mkoa wa Kigoma na nchi jirani ya Burundi ili kutoa fursa kwa vijana kupata ajira kupitia tasnia hiyo.
Mara baada ya kupokea Mipira hiyo, Andengenye amemshukuru Ndikuriyo kwa Moyo wake wa Uzalendo unaomsukuma kuguswa na mustakabali wa kizazi kilichopo na kijacho na kuandaa njia za mafanikio kupitia michezo pamoja na kuendelea kuimarisha mahusiano mema baina ya nchi za Tanzania na Burundi.
Upande wake balozi huyo katika ubalozi mdogo wa Burundi nchini Tanzania amesema nchi yake itaendelea kuheshimu udugu uliopo baina ya mataifa hayo mawili huku akisisitiza kuunga mkono juhudi za Ndikuriyo katika kukuza Sekta ya michezo ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
‘’Mpira umekuwa chanzo chanzo cha ajira na kutoa fursa za kujiinua kiuchumi kwa vijana ndani na nje ya nchi zetu, hivyo tukiimarisha msingi huo kwa kuwawezesha vijana tutawasaidia kufikia malengo yao kupitia mchezo wa Soka’’ amefafanua Jeremie.
Kupitia kikao cha Maandalizi ya Ligi ya Ujirani mwema inayohusisha Mkoa wa Kigoma na mikoa ya Burundi inayopakana na Tanzania mwaka 2022, wajumbe walikubaliana ligi hiyo ihusishe vijana wenye Umri wa chini ya Miaka 18 kwa lengo la kuibua vipaji na kuhamasisha mchezo huo kwa vijana.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa