Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka Maafisa Utumishi katika Halmashauri mkoani humo kushughulikia changamoto za kiutumishi zinazowakabili watumishi wa Umma ili kuondoa manung’uniko yanayochangia kushusha ari ya kiutendaji kwa wafanayakazi.
Ujio wa kauli hiyo umefuatia Mkuu huyo wa Mkoa kukutana na watumishi wa Umma katika Halmashauri ya wilaya ya Kakonko akiwa kwenye ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua miradi ya Maendeleo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
‘’ Msiruhusu watumishi wa Umma wakaacha majukumu yao kwa lengo la kuwafuata kwenye ofisi zenu, hali hii inasababisha kupoteza muda mrefu wanaopaswa kuutumia kutekeleza majukumu yao’’alisema.
‘’Mnafahamu dhamana yenu katika utumishi wa Umma hivyo wapunguzieni kazi ya kuhangaika kutafuta viongozi au watu wa kuwasaidia kutatua matatizo ambayo yapo chini ya uwezo wenu’’ alisistiza Andengenye.
Katika kuhakikisha agizo hilo linafanikiwa kiutekelezaji Mkuu huyo wa Mkoa amewaelekeza wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanawawezesha maafisa utumishi kuwafikia watumishi wa Umma katika maeneo ya kazi ili kuwasikiliza na kutatua changamoto zinazohitaji miongozo ya kiutumishi.
Akizungumzia utendaji kazi wenye tija, kiongozi huyo amewataka watumishi wa Umma mkoani hapa kudumisha uadilifu, nidhamu na kujituma ili waweze kupata matokeo makubwa katika utendaji kazi wao.
‘’Niwasihi tuendelee kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita kwa kutangaza kazi nzuri zinazofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu huku tukikumbuka sisi sote ni wasaidizi wake katika kuwatumikia wananchi na kuliletea Maendeleo Taifa letu’’ ameongeza.
‘’Mkitumia vibaya nafasi zenu mtaleta matokeo hasi kwa Taifa letu hivyo shirikianeni, pokeeni ushauri na maelekezo kutoka kwa viongozi wenu pamoja na kutanguliza uzalendo katika utendaji kazi wetu’’ametahadharisha Mkuu huyo wa Mkoa.
Kupitia ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amekagua ujenzi wa Shule ya Sekondari Rutenga inayojengwa kwa fedha kiasi cha Shilingi 603,890,562 kutoka Serikali Kuu pamoja ujenzi wa miundombinu katika shule ya msingi Nyamwilonge chini ya Mradi wa BOOST kwa Thamani ya shilingi 110,600,000 pamoja na Shule ya Kumkobe Shilingi 361,500,000.
Upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ndaki Mhuli amesema kukamilika kwa shule hizo kutapunguza Adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kielimu.
Pia Ndaki amewataka wazazi katika kata ya Nyamtukuza kutumia miundombinu hiyo kuendana na malengo ya serikali ili kuhakikisha watoto wote katika maeneo hayo wanapata elimu bora.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa