Na. Clinton Justine-Kigoma.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Magharibi yaliyohusisha Mikoa ya Tabora na Kigoma yamehitimishwa Tarehe 8, Agosti, 2025 ambapo kutokana na umuhimu wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Balozi Simon Sirro aliongeza Siku mbili ili wadau wa maonesho hayo kupata fursa Zaidi ya kunufaika na tukio hilo.
Kupitia maonesho hayo imeshuhudiwa wafugaji, wakulima, wadau wa uvuvi, mashirika, Kampuni na Taasisi mbalimbali za kibiashara na kifedha pamoja na wajasiriamali wakijumuika kuonesha, kutangaza na kuuza bidhaa zao sambamba na kutoa maelekezo ya namna huduma wanazotoa zinavyoweza kuleta mapinduzi katika maisha ya kila siku ya binadamu.
Pamoja na yote hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma akiwa mgeni rasmi katika kufunga maonesho hayo amesisitiza mambo kadhaa ikiwemo suala la kuanzishwa kwa madarasa maalum yatakayohusisha wataaalam kutoka Idara, vitengo au ndani ya Sekta mbalimbali kwa lengo la kuwakutanisha pamoja wananchi na kuwafundisha namna bora ya kutekeleza majukumu yao kuendana na Sekta waliyojikita kiuzalishaji.
Anasema mfano; kukiwa na eneo maalum la darasa, wahitaji wataenda hapo na kupatiwa mafunzo bobezi ndani ya siku husika za maonesho. Mfano Idara ya Uvuvi itaandaa mtaalam bobezi kutoka katika Wizara hiyo naye atatengewa eneo maalum kwa ajili ya kuwafundisha wadau wa uvuvi hatua kwa hatua na kwa kina kuhusu shughuli za uvuvi wanazozifanya ili nao wakitoka hapo waweze kwenda kuwa walimu wazuri kwa jamii katika maeneo yao ya uzalishaji.
Anasema sambamba na hayo, Halmashauri zinapaswa kuandaa utaratibu wa kuchukua sampuli za wadau wa nanenane kama wafugaji, wafanyabiashara wadogowadogo, wazalishaji wadogo au wale wa kati na hata wakulima kisha kuwaweka kwenye madarasa hayo ili kuwajengea uwezo kwa makubaliano ya kwenda kutoa elimu hiyo katika maeneo yao.
Pamoja na hayo, Mkuu wa Mkoa ameenda mbali Zaidi kwa kuzitaka halmashauri na taasisi zinazohusika katika shughuli za maonesho katika maeneo yao kuhakikisha zinajenga miundombinu ya kudumu na yenye mifumo rafiki kwa ajili ya kazi wanazozifanya.
Aidha kupitia hotuba aliyoitoa kwenye kilele cha maadhimisho hayo, Mhe. Balozi Sirro ametoa wito kwa wakulima wafugaji na wavuvi kuongeza kasi ya matumizi ya teknolojia, zana bora na za kisasa pamoja na kujifunza na kwenda sambamba mnbcxvz na mifumo ya kisasa ya ufugaji ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Aidha Balozi Sirro amezungumzia umuhimu wa kuboresha kwa kiasi kikubwa mifumo ya uandaaji wa vifungashio ili kuziweka bidhaa katika hali ya kuhimili ushindani wa kimasoko. Anasema iwapo bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa katika soko la dunia hazitokuwa na vifungashio vyenye kuzitambulisha bidhaa hizo zitakosa soko la uhakika na zitaishia kuuzwa katika soko la ndani.
‘’Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wenzetu wa Shirika la Viwango Tanzania(TBS) kuona namna bora ya kushiriki maadhimisho haya kwa mwaka ujao ili watupe mkakati na kutoa Elimu ya namna bora ya kupata huduma ya wataalam wa vifungashi na kuziwezesha bidhaa zetu kuingia katika masoko makubwa ya ndani sambamba na kuleta ushindani katika Soko la Dunia’’ ameshauri Sirro.
Kwa kuongezea amezitaka Halmashauri kwa kushirikiana na wataalam wa Sekta ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji kuanza mchakato wa kuwajengea uwezo wananchi wazalishaji kuhusu umuhimu wa kutumia vifungashio vinavyokidhi viwango vya kimataifa sambamba na kuwakutanisha na wataalam watakaowasaidia namna bora ya kufanikisha upatikanaji wa wataalam wanaohusika na zoezi hilo.
Awali Hassan Rugwa ambaye ni Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma alitembelea mabanda hayo na kuzungumza na wadau wa nanenane ambapo aliwasisitiza kuhakikisha wanatumia fursa ya maonesho hayo sio tu kwa kutangaza bidhaa zao bali kuziuza.
‘’Kiuhalisia ili tufikie malengo yetu ni lazima bidhaa tunazoleta kuzitangaza ziwe na ubira na zenye utofauti ili ziweze kumudu ushindani wa kimasoko sambamba na kuuzika kwa wingi. Mtakapokuja tena kwenye maonesho haya mwaka ujao hakikisheni mnasafirisha bidhaa zenu kwa ajili ya kuziuza pia badala ya kuishia kuzitangaza’’ ameshauri Rugwa.
Kuhusu ushindani wa kimasoko, Katibu Tawala huyo amewataka wataalam wa Halmashauri katika Sekta ya Biashara kuzidi kutumia teknolojia ya kisasa kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuwapunguzia adha wananchi wazalishaji mali ambao wanauhitaji mkubwa wa amsoko hayo kutokana na kufanikia katika uzalishaji wa bidhaa.
Mkoa wa Kigoma na Tabora kwa ujumla ni mikoa yenye kiwango kikubwa cha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa wingi sambamba na uwepo wa mazao ya uvuvi pamoja nay ale yatokanayo na Nyuki. Mazao haya yameendelea kuwa na soko kubwa ndani nan je ya nchi, hivyo Rai ya Mkuu wa Mkoa kuhusu matumizi ya vifungashio sahihi na vyenye kukidhi viwango vya kimataifa ni jambo lisilokwepeka ili kuinua pato na kuleta matokeo chanya kwa mkulima.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa