Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa ameitaka Jamii mkoani hapa kuchangamkia fursa ya Elimu ya Fedha inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha ili kuwajengea wananchi uelewa na kudhibiti athari za kiuchumi zitokanazo na ukosefu wa Elimu ya uwekezaji, utunzaji wa akiba na mikopo isiyo na tija.
Rugwa ametoa wito huo alipokutana na kufanya mazungumzo na wataalam kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI waliopo mkoani hapa kwa lengo la kutoa mafunzo ya Elimu ya Fedha kwa makundi mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara, watumishi wa Umma na Sekta Binafsi, wajasiriamali, watoa huduma za kifedha, wawekezaji, SACCOS, vikundi vya kifedha vya kijamii pamoja na wanufaika mbalimbali wa huduma za kifedha mkoani hapa.
Amesema Elimu ya Fedha ni suala muhimu kwa kila mnufaika wa fedha ili kupata ujuzi wa kuhifadhi, kuziendeleza, kufahamu Sheria za biashara, ulipaji kodi, taratibu za uwekezaji na upatikanaji wa hisa sambamba na kufanya matumizi binafsi yatakayolenga kuheshimu matumizi bora ya fedha.
Ameeleza kuwa, kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi kupata ujuzi wa Elimu ya Fedha na Biashara, ili kuwajengea uwezo na kuwaongezea ubunifu wananchi katika kufanya biashara pamoja na uwekezaji na kujiongezea kipato hali itakayosaidia kuepuka hasara zisizo za lazima.
‘’Kigoma ni miongoni mwa mikoa inayotoa idadi kubwa ya wajasiriamali ndani na nje ya mkoa hivyo suala hili limekuja katika muda sahihi kwani itasaidia kuwajengea uelewa wale walipo kwenye biashara katika ngazi mbalimbali pamoja na wanaofikiria kuanzisha biashara’’ alisema Rugwa.
Upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Stanley Kibakae amesema lengo ni kutembelea na kukutana na wanufaika wa fedha katika Halmashauri zote za Mkoa wa Kigoma ili kuwajengea uwezo watoaji na wapokeaji wa huduma za kifedha.
Amefafanua kuwa mkoa wa Kigoma hali ya uelewa wa masuala haya ya kifedha ipo chini ndio maana Wizara imechukua hatua ya kutuma wataalam watakaokutana na wadau wa fedha na kuhakikisha Elimu inayotolewa inabadilisha mitazamo na uelewa wa kifedha kwa makundi mbalimbali.
Amesema Elimu ya fedha ni Taaluma ya kielimu kama zilivyo elimu nyingine hivyo lengo ni kuleta mabadiliko, aidha amesisitiza kuwa, utoaji wa elimu umerahisishwa ili kila atakayefikiwa aweze kuwa na uelewa na kumudu kuendana na Sheria ya huduma ndogo za kifedha ya Mwaka 2018 na kanuni yake ya Mwaka 2019.
‘’Kuna baadhi ya watoa huduma za kifedha wanakumbwa na changamoto za kukosa uelewa wa masuala yakifedha au kukosa uaminifu jambo linalosababisha kutoza riba kuwa na kuweka masharti yasiyo rafiki na kandamizi dhidi ya wapokea huduma za kifedha’’ alisema Kibakae.
Ameongeza kuwa elimu hiyo ni muhimu ili kuhakikisha wanufaika wa kifedha wanafanikiwa kuweka akiba, kufanya uwekezaji, kufahamu taratibu za kulipa kodi sambamba na kutoa fursa kwa wafanya kazi kujiandaa na maisha baada ya kutamatika kwa muda wao wa kiutumishi.
Kadhalika kupitia maarifa hayo ya kifedha, watoa huduma za kifedha watasajiliwa na kutambuliwa rasmi,watendana na sharia za nchi zinazoongoza taratibu za kifedha, ‘’nitoe wito kwa wajasiriamali na wafanyabiashara mkoani Kigoma kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuendana na sheria ndogo za fedha’’ alisisitiza Kibakae.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa