Wakazi katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji wametakiwa kutunza na kuilinda Miundombinu ya Maji iweze kudumu na kuinufaisha Jamii kwa Muda mrefu ili Fedha zinazotengwa kwa ajili ya ukarabati zikatumike kuendelezana kuibua miradi mingine.
Miundombinu ya Maji iliyopo ikitumiwa kwa usahihi na kuiepusha na uharibufu, itaruhusu pesa zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati kutumika katika kuendelea kuisogeza huduma hiyo muhimu katika maeneo ambayo hayajafikiwa na kuzidi kuigusa idadi kubwa ya wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amesema hayo alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa chanzo cha Maji cha Amani Beach akiambatana na Katibu Tawala pamoja na Kamati ya Ulinzi Mkoa, kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wa Chanzo hicho kipya cha Maji katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Amesisitiza kuwa iwapo miundombinu hiyo itatunzwa, Marekebisho yatafanyika katika maeneo yenye uchakavu na ubovu na sio kwa sababu ya uharibifu wa makusudi unaofanywa na watu wachache wenye nia ovu dhidi ya mipango ya Maendeleo ya Serikali.
‘Tukiilinda na kuitunza miundombinu tuliyonayo, tutapunguza gharama za kuendesha mradi na kupanua wigo wa utoaji wa huduma, hivyo yeyote atakayebainika kufanya uharibifu hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo’’ amesisitiza Andengenye.
Aidha Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza fursa ya wananchi kuunganishwa katika mfumo wa Huduma ya Maji na kutimizwa kwa azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kumtua mama ndoo kichwani.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Kigoma/Ujiji Mha. Mbike Jones amesema mradi huo umekamilika na tayari unazalisha lita Mil. 23 kwa siku huku mahitaji halisi ikiwa ni Lita Mil. 23 hivyo kufanya uzalishaji kufikia Asilimia mia moja.
Amefafanua kuwa Mradi huo ulianza kutekelezwa Julai 2021 na na kukamilika Januari 2023 chini ya Mkandarasi Sinohydro Corporation Ltd, unauwezo wa kuzalisha Mita za ujazo 42,000 kwa siku na unanufaisha takribani watu 384,000 wakazi wa Manipsa ya Kigoma/Ujiji na maeneo ya Jirani.
Aidha amewasisitiza wateja wa Huduma hiyo kulipa madeni ya Huduma ya Maji wanayodaiwa kwa wakati ili kuruhusu uendeshaji wa uhakika wa Mradi huo.
‘‘wateja wetu wanapolipa madeni yao Fedha tunayoipata inatuwezesha kununua vipuri, kukarabati mitambo pamoja na miundombinu ili kuifanya huduma ya Maji kuwa ya uhakika’’ amesisitiza Mha. Mbike.
Pia Mha. Mbike amefafanua kuwa hali ya kuwepo kwa mgao wa Maji kwa Baadhi ya maeneo inatokana na mabomba kutokuwa na uwezo mkubwa wa kupitisha maji hivyo katika kutatua changamoto hiyo, mamlaka inampango wa kuyafikia kisha kuyatambua maeneo hayo kwa lengo la kubadilisha aina ya mabomba yanayotumika.
‘‘Nitoe Rai kwa wananchi wote wenye uhitaji wa huduma ya Maji watume maombi katika sehemu husika ili waweze kupatiwa huduma hiyo kwani uzalishaji ni toshelevu na unaendana na idadi halisi ya mahitaji katika manispaa ya Kigoma/Ujiji na maeneo jirani’’ amesema Mhandisi Mbike.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa