Ukosefu na kutoimarika kwa Huduma za Mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mahakama nyingi nchini kumetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuchelewesha mchakato wa kushughulikia Mashauri ya Kimahakama.
Kauli hiyo imetolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Ibrahim Juma alipofungua kikao kati ya Tume hiyo, watumishi wa Mahakama pamoja na Kamati za Maadili uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma.
‘’Pamoja na kuanzishwa kwa Mifumo wa Kitekonolojia, Mahakama nyingi nchini hazijaunganishwa na Mifumo madhubuti ya TEHAMA itakayowezesha kuratibu na kuendesha kesi kwa njia ya mtandao’’ amesema Jaji Prof. Juma.
Jaji Juma amezitaja pia changamoto za uhaba wa watumishi katika Mahakama mpya, ukosefu wa Huduma ya Magereza katika Wilaya Mpya pamoja na ukosefu wa Umeme wa uhakika kwenye majengo ya Mahakama, kuendelea kuchangia katika kuchelewesha mienendo ya kesi nchini.
Kupitia Taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za Kamati ya Maadili Mkoa wa Kigoma aliyoiwasilisha kwenye Mkutano huo, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Maadili Mkoa Albert Msovela amesema Mkutano huo utaamsha ari ya kiutendaji kwa Kamati ya Maadili Mkoa na za Wilaya.
Amesema Kamati zote hazijapokea malalamiko dhidi ya utendaji kazi wa watumishi wa Mahakama katika ngazi mbalimbali kutokana na watendaji hao kutawaliwa na weledi na maadili ya kiutumishi katika utendaji kazi wao.
Aidha amesisitiza kuwa, kutokuwepo kwa malalamiko ya wananchi dhidi ya watendaji wa kimahaka kumechangiwa na kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa wakazi kuhusu masuala ya kisheria pamoja na taratibu za Mahakama.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Kanda ya Iringa Ilvin Mgeta amesema Kamati za Maadili zinaendelea kusimamia Jukumu la kuhakikisha maadili yanazingatiwa na watumishi wa Mahakama kwa kupokea na kufanyia kazi malalamiko ya Wananchi dhidi ya changamoto za upatikanaji wa Haki kwa wananchi.
Aidha amewasisitiza watumishi wa Mahakama kwa ngazi zote nchini kuhakikisha wanatoa huduma kuendana na miongozo ya kisheria iliyowekwa na Serikali kwa lengo la kuepuka ukosefu wa haki unaosababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa