Dkt. Suleiman Daud akitoa neno la shukurani kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma( hayupo pichani) Mara baada ya kumaliza mazungumzo mafupi yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma. Dkt Daudi akiambatana na wataalam kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali wamefika mkoani Kigoma kwa lengo la usimamizi wa utekelezaji katika Mradi wa ujenzi wa Chuo cha TEHEMA Wilaya ya Buhigwe.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati inayoundwa na Wataalam kutoka taasisi za Serikali waliofika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma wakifuatilia maelezo ya Mkuu wa Mkoa, Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye.
‘’Wawekezaji wengi wanashindwa kuungana nasi ili kuwekeza katika Mkoa wa Kigoma kutokana na tatizo kukosekana kwa uUmeme wa kutosha wenye uhakika. Lakini tunaelekea kuzuri kwani Serikali yetu chini Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutekeleza Miradi mikubwa ya Umeme mkoani hapa’’ amesema Andengenye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Amesema hayo alipokutana na Timu ya Wataalam kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali, iliyopo mkoani hapa kwa Lengo la usimamizi wa utekelezaji Mradi wa ujenzi wa Chuo cha TEHAMA katIka Wilaya ya Buhigwe.
Amesema kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Mradi wa Umeme wenye Kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kidahwe katika Wilaya ya Kigoma vijijini ambapo kukamilika kwa mradi huo kutamaliza kabisa adha ya Umeme mkoani hapa na kufungua fursa za uwekezaji hasa wa viwandani.
Dkt. Suleiman Daud kiongozi wa Timu ya Wataalam toka Taasisi za Serikali, amesema Kigoma ni Mkoa wa kimkakati hususani katika suala la Elimu kutokana na kupakana na Nchi za jirani, hivyo mahitaji ya umeme ni muhimu kwani yanapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya Teknolojia.
Amesisitiza kuwa, ujenzi wa chuo cha TEHAMA utafungua fursa kwa watanzania na Raia wa Kigeni kusoma katika chuo hicho, hivyo Miundombinu wezeshi ni muhimu katika kufikia malengo hayo.
‘’Tunaimani na Uongozi wa Mkoa pamoja na wilaya ya Buhigwe kwani viongozi waliopo ni mahiri na tunauhakika kuwa zoezi la Ujenzi wa chuo hicho litapata usimamizi wa kutosha na kukamilika kwa wakati’’ amesisitiza Dkt. Daud.
Chuo hicho kinatarajiwa kujengwa katika Kijiji cha Songambele wilayani Buhigwe Mkoani hapa, ambapo tayari wananchi wa Buhigwe wamekubali kutoa eneo la Ekari 149.9 kwa ajili ya ujenzi huo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa