Kituo cha kuratibu Mfumo wa Huduma ya Usafiri wa Dharura kwa wajawazito, Mama na watoto wachanga (m-mama) umezinduliwa rasmi mkoani Kigoma na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Dkt. Jesca Lebba amewataka watendaji watakaohusika na uendeshaji wa mfumo huo kutanguliza uzalendo kwani ufanisi wake utachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo kwa wajawazito, wazazi na watoto.
Amesema mahitaji ya usafiri ni makubwa kwani magari hitajika kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa kimkoa ni 50, ambapo yaliyopo ni 24 huku upungufu ikiwa magari 26 sawa na asilimia 52.
Upande wake Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma Dkt. Stanley Binagi amesema ukosefu wa usafiri wa uhakika umekuwa ni changamoto iliyosababisha vifo vingi kwa makundi hayo hivyo ujio wa mfumo huo utapunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya vifo vya wanawake, wajawazito na watoto wachanga.
Ameendelea kusisitiza kuwa, kwa kushirikiana na wadau wa Huduma ya m-mama, watahakikisha Mfumo unafanya kazi wakati wote kutokana na Hospitali kupokea na kutoa huduma kwa wagonjwa wote wanaopewa rufaa kutoka Hospitali za wilaya mkoani Kigoma.
‘’Ili kutimiza malengo ya kuanzishwa mfumo wa m-mama, watendaji wanapaswa kushirikiana na kuhakikisha mfumo unakuwa wazi kiutendaji kwa Saa 24 kila siku ili uweze kutoa huduma nyakati zote’’amesema Dkt. Binagi.
Mfumo wa m-mama unaendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau ambao ni Vodacom, Touch Foundation pamoja na Pathfinder International.
Huduma ya m-mama mkoani Kigoma inapatikana kwa kupiga Namba ya Huduma 115 na wananchi wanashauriwa kutumia namba hiyo kwa dharura zinazohusu walengwa ili kuepusha hasara na matumizi yasiyo ya lazima kwa rasilimali za Serikali na upotevu wa muda kwa watendaji.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa