PICHA: BAADHI YA MIRADI ILIYOTEMBELEWA NA TIMU YA UTAYARISHAJI WA KIPINDI CHA TAMISEMI KAZINI MKOA WA KIGOMA.
Ujenzi wa Nyumba Tano za watumishi wa Idara ya Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu. Ujenzi huo unaotekelezwa kutokana na Fedha za Mapato ya Ndani unna lengo la kupunguza adha kwa watumishi wa Hospitali hiyo kukaa mbali na Kituo cha kazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Ujenzi wa Jengo la kudhibiti Magonjwa ya Mlipuko (Isolation Centre) katika Kituo cha Afya Nyakitoto Wilayani Kasulu.
Kitalu cha Miche ya zao la Chikichi kilichopo katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji.
Kituo cha Afya Buhanda Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Katika kuhakikisha Umma unahabarika na kupata taarifa mbalimbali za kazi zinazofanywa na Serikali, Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) imeanzisha Kipindi Maalum cha Televisheni Kiitwacho TAMISEMI KAZINI.
Bi Angela Msimbira Afisa Habari Mkuu TAMISEMI anayeongoza Timu ya utayarishaji wa kipindi hicho, amesema walengwa wa kipindi ni Wananchi ambao wanataka kufahamu matumizi ya kodi zao kupitia shughuli mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa na Serikali kwa lengo la kuwaletea Maendeleo.
Afisa habari huyo amesema wameridhishwa na ushirikiano waliopewa na Wakurugenzi pamoja na wakuu wa Idara katika zoezi la kutembelea miradi iliyopendekezwa kutembelewa kwa ajili ya upigaji picha pia ushiriki mzuri katika utoaji wa taarifa kupitia mahojiano yaliyofanyika kwa lengo la uandaaji wa kipindi.
Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameipongeza Wizara ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI kwa kuanzisha kipindi hicho Maalum cha Runinga ambacho kitawafanya wananchi kufahamu kazi zinazofanywa na Serikali na kupunguza sintofahamu kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa pongezi hizo mara baada ya kumaliza sehemu yake katika maandalizi ya kipindi hicho ambapo ameshirki katika mahojiano yaliyofanywa na Nguli wa uandaaji wa vipindi na utangazaji, Asheri Thomas kutoka Shirkia la Utangazaji la Taifa.
‘‘Nimefurahishwa na uanzishwaji wa kipindi hiki, kwani kitasaidia kuwafahamisha wananchi kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na Serikali zikiwa na lengo la kuboresha maisha yao na kuwafanya waishi katika kiwango bora’’ amesema Andengenye.
Zoezi hilo limefanyka katika Manispaa ya Mji Kigoma-Ujiji, kisha kuendelea katika Wilaya za Kasulu na Uvinza ambapo miradi mbalimbali imetembelewa kupigwa picha na kufanyika kwa mahojiano.
Aidha kipindi hicho kimelenga kuangazia taarifa za ukusanyaji wa mapato ya ndani , utoaji wa mikopo ya Asilimia Kumi na Miradi inayotekelezwa kwa fedha zitokanazo na mapato ya ndani.
Mkoa wa Kigoma umechaguliwa kuwa wa kwanza katika uandaaji wa Kipindi cha TAMISEMI KAZINI kinachotarajiwa kuanza kurushwa hewani na kituo cha Runinga cha Taifa (TBC ONE).
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa