TANI 2,521,038 ZA CHAKULA ZILIZALISHWA MKOANI KIGOMA MSIMU WA 2023/2024
-Serikali yaahidi kuendelea kushirikiana na wadau kuimarisha kilimo boashara.
-Mkoa kuwa kitovu cha uzalishaji wa mazao ya chakula ukanda wa magharibi na nchi jirani kwa kuzalisha zaidi ya Tani Mil.2.1
-Mikakati ya ujenzi wa Skimu za umwagiliaji yaendelea ili kuwatoa wananchi katika kutegemea kilimo cha msimu.
MKUU WA MKOA WA KIGOMA MHE. THOBIAS ANDENGENYE (KULIA) AKIPIGA MAKOFI MARA BAADA YA KUKABIDHI GARI KWA KATIBU TAWALA MKOA WA KIGOMA MHE. HASSAN RUGWA KWA AJILI YA URATIBU WA SHUGHULI ZA KILIMO MKOANI KIGOMA.
Kuelekea msimu wa Kilimo wa 2024/2025 Serikali ya mkoa wa Kigoma itaendelea kushirikiana na wadau wa Maendeleo kwenye Sekta ya Kilimo kupitia kuweka mkazo katika kuboresha mifumo ya uzalishaji kupitia na kuhakikisha wakulima wanalima kwa kuzingatia kanunia za kilimo bora kupitia usimamaizi wa maafisa ugani Kilimo waliopo katika halmashauri zote za Mkoa wa Kigoma.
Ifahamike kuwa, takribani Tani zipatazo 2,144,058 za Mazao ya Chakula zimezalishwa mkoani Kigoma kwa msimu wa Kilimo 2023 hadi 2024 ambapo jumla ya Hekta 899,388 zimelimwa na kuufanya mkoa kuwa na chakula cha kutosha.
Ikumbukwe kuwa, Mkoa wa Kigoma umeendelea kuwa miongoni mwa mikoa kinara kwa uzalishaji wa mazao ya Chakula hali inayosababisha wakazi kuondokana na changamoto ya uhaba wa chakula sambamba na kufanikiwa kuchangia chakula kwa mikoa na nchi jirani za Burundi, Rwanda, Congo DR na Uganda.
Mfano kwa Msimu wa 2022/2023, jumla ya Hekta 905,035.92 sawa na 92% zililimwa na mkoa kufanikiwa kuzalisha takribani tani 2,734,367.98 ya mazao ya chakula na kupelekea mkoa kuendelea kuwa na hali ya utengamano katika usalama wa chakula.
Ili kuendelea kuimarisha kasi ya uzalishaji wa mazao ya chakula, mkoa unaendelea kuwasisitiza wakulima na wananchi kwa ujumla kuzingatia matangazo maelekezo ya wataalam wa Kilimo na utabiri unaotolwa na mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA)sambamba na kuepuka kuuza akiba ya chakula walichinacho bila kuwepo kwa sababu za msingi.
Aidha elimu ya kilimo cha kisasa inaendelea kuwafikia wananchi kwani kwa kuthibitisha hilo mkoa ni miongoni mwa mikoa ambayo matumizi ya pembejeo kwa wakulima yameongezeka kwa kasi kubwa ambapo msimu wa 2022/2023 matumizi ya mbolea yalifika wastani wa tani 31,557 huku msimu 2023/2024 yakifikia tani 32,198.
Afisa Kilimo mkoa wa Kigoma Peter James anasema kuelekea msimu wa 2024/2025 takwimu zinaonesha mahitaji halisi ya mbolea yamefikia hadi tani 42,502 sawa na ongezeko la asilimia 13.8 ikilinganishwa na mahitaji ya msimu wa 2023/2024.
Anasema pamoja na changamoto za mkoa kuwa na eneo kubwa la kiutawala, wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana na mamalaka za kiserikali zinazosimamia masuala ya kilimo ili kuhakikisha wanafanya kilimo chenye tija ambacho kitawafanya kufikia lengo la serikali la kilimo cha kibiashara.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye anakiri kwamba mwamko huo wa matumizi ya pembejeo za kilimo umechagizwa na kasi kubwa ya utoaji wa elimu ya utunzaji wa Mazingira kwa wakulima kupitia kuepuka Kilimo cha kuhamahama na kuzingatia kanuni na Sheria za matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya vijiji.
Aidha Andengenye amesisitiza kuwa, mabadiliko hayo hayakuja yenyewe bali yametokana na msingi mkubwa uliowekwa na serikali katika kuhakikisha Maendeleo ya Kilimo yanafikiwa, Jambo linalosimamiwa vizuri na Wizara ya Kilimo kupitia usambazaji wa kutosha wa mbolea katika Halmashauri zote za mkoa.
‘’Serikali ya Awamu ya Sita kupitia uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu imefanikiwa kuongeza idadi ya mawakala katika vituo vya kuuzia mbolea ya ruzuku kutoka vituo vitano (5) kwa msimu wa 2022/2023 hadi kufikia 87 kwa msimu wa 2023/2024, jambo linaloendelea kuzogeza na kupunguza adha ya upatikanaji wa huduma za pembejeo mkoani Kigoma’’ anasema Mkuu wa Mkoa.
Aidha Serikali ya Mkoa wa Kigoma katika kutekeleza mkakati wa Tanzania kuwa ni nchi ya viwanda na uchumi wa kati, imefanikiwa kutangaza zao la chikichi, Pamba, Kahawa, Tumbaku, Chai, Korosho, Mkonge na Alizeti kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati.
Sambamba na hayo, serikali imeendelea kusimamia uzalishaji wa mazao ya chakula kama vile Mpunga, Maharage, Mahindi, Muhogo, viazi, na mazao mengine ya mbogamboga ili kukabiliana na uwezekano wa kuibuka kwa tatizo la uhaba wa chakula kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma.
Katika kuhakikisha kilimo endelevu kisichotegemea majira ya mvua, Wizara ya Kilimo kupitia Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) amekabidhi mradi wa umwagiliaji Bonde la Luiche lenye ukubwa wa hekta 3000, ambapo utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya kutimiza maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza kilimo cha umwagiliaji nchini.
Sambamba na mradi huo, wizara ya Kilimo inaendelea na usanifu katika wilaya ya Buhigwe, Kasulu Vijijini na Kakonko kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miradi mikubwa ya Skimu za umwagiliaji ili kuwatoa wananchi katika mfumo wa kilimo cha msimu.
Mkoa umeendelea kuimarisha mnyororo wa Thamani katika mauzo ya mazao ya kilimo ambapo kwa kushirkiana na wadau mbalimbali wa Kilimo kama Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (Enabel) wananchi wamejengewa uwezo katika mfumo wa kilimo biashara ikiwemo uzalishaji, usindikaji na upatikanaji wa masoko kwaajili ya kuuza mazao kwa bei yenye tija kupitia vikundi vya wakulima.
Wito wa uongozi wa Mkoa kwa wakulima ni kuhakikisha wanaendelea kuwatumia maafisa ugani Kilimo waliopo maeneo yao kwa ajili ya kupata ushauri kuhusu aina ya kilimo wananchotaka kukifanya sambamba na kuzingatia miongozo na kanuni bora za kilimo cha kisasa kwa ajili ya mazao ya biashara na yale ya chakula ili kuendelea kudhibiti changamoto ya uhaba wa chakula pamoja na kujiimarisha kiuchumi.
Aidha Mkoa unaendelea kuwaalika wawekezaji katika Sekta ya Kilimo kutokana na uwepo wa maeneo na mazingira ya jumla yanayoruhusu kufanyika kwa uwekezaji huo kiwemo maboresho makubwa ya miundombinu ya barabara zinazouunganisha mkoa na mikoa pamoja na nchi jirani, mkoa kuunganishwa umeme wa gridi ya Taifa, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na kuimarika kwa masoko ya kimkakati yanayoendelea kuchechemua uchumi wa wakazi wa mkoa na maeneo jirani.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa