Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka watendaji katika Taasisi za Umma na Halmashauri mkoani hapa kuongeza ubunifu katika kubaini vyanzo vya mapato ili kuongeza kuinua kiwango cha makusanyo katika Halmashauri na kuziwezesha kumudu kujiendasha sambamba na kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Mhe. Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza kwenye Kikao kilichowakutanisha wataalam kutoka Taaasisi za Umma pamoja na watendaji kutoka mamalaka za serikali za mitaa mkoani hapa kikilenga kujadili na kubaini fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo kwenye mkoa wa Kigoma na kupanga mikakati ya namna bora ya kuzitumia ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Amesema mko una vyanzo vingi vya Mapato, kinachotakiwa ni ubunifu katika ubainifu wa vyanzo hivyo ili viweze kuleta tija katika uzalishaji na ukusanyaji wa mapato, jambo litakaloimarisha uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watendaji hao kujenga utamaduni wa kutoa huduma bora kwa wananchi jambo litakalowezesha wapokea huduma kuzitangaza kazi nzuri zinazofanywa na serikali mkoani hapa.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu huyo wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema lengo la kikao hicho ni kufanya mapitio ya vyanzo vya mapato vya taasisi za Umma mkoani hapa na kuona namna bora ya kuongeza makusanyo ya ndani.
Amesema malengo ya mkoa ni kuhakikisha kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2024/2025 malengo ya makusanyo kimkoa hadi ifikapo 20230 ni kufikia kati ya shilingi Bil.20 hadi 25.
Aidha Rugwa amewataka watendaji hao kwenda kuibua vyanzo vipya vya mapato katika maeneo yao wanayoyasimia na kuondoa vyanzo visivyo na tija.
‘’Hakikisheni mnaandaa mazingira bora ya ukusanyaji wa mapato, kuondoa tozo zinazoweza kuwaletea kero wananchi sambamba na kuandaa mazingira yatakayotoa fursa kwa wawekezaji ili waweze kuwekeza katika maeneo yenye vivutio vya uwekezaji’’ amesema Rugwa.
Upande wake Mkuu wa Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa Ndg. Deogratius Sangu amesema kikao hicho cha wataalam wa mkoa kimehusisha wakuu wa Taasisi za Umma zilizopo mkoani humo, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, wachumi, wataalam wa mipango na mipango miji pamoja na Maafisa biashara lengo kuu likiwa kuhakikisha wataalam hao wanajengewa uwezo katika kubaini na kuhakikisha wanatumia vursa za kiuchumi zilizopo mkoani humo kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa