Watendaji wa Serikali mkoani Kigoma wametakiwa kuzingatia Miongozo ya matumizi ya Fedha za Umma ili kufanikisha mipango ya Serikali inayolenga kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa alipozungumza katika hafla fupi ya kimkoa mara baada ya kukabidhiwa tuzo ya umahiri katika Uandaaji wa Hesabu za Fedha kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uhasibu Sekta ya Umma kwa mwaka 2022/2023 iliyotolewa na bodi ya Taifa ya wahasibu na wakaguzi Tanzania (NBAA) ambapo mkoa umeshika nafasi ya tatu kipengele cha mikoa.
Amesema katika namna ya pekee anatoa pongezi kwa watendaji wote kwa ushirikiano wao uliosababisha mkoa wa Kigoma kuendela kushika nafasi za juu kwa kipindi cha miaka sita.
"Kwetu tuzo hii inatoa tafsiri pana na kuonesha kuwa tunatekeleza majukumu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Matumizi ya Fedha kuanzia upangaji wa bajeti na mlolongo wa utekelezaji wa bajeti hiyo katika mkoa na mamlaka za Serikali za Mitaa" amesisitiza Rugwa.
Aidha amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuufungua mkoa ikiwemo kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za jamii jambo litakalotoa fursa kwa wananchi kupata huduma bora sambamba na kuzidi kufungua fursa za kiuchumi.
Johson Gamba, Muhasibu Mkuu wa Mkoa amesema mkoa umeendelea kupata tuzo hiyo kwa miaka sita ikiwa ni ishara ya uongozi wa mkoa wa Kigoma kusimamia vizuri fedha zinazotolewa na serikali katika kutekeleza kazi na miradi mbalimbali ya Maendeleo.
"Ni vizuri watendaji wote tunaohusika na matumizi ya fedha ngazi ya mkoa na halmashauri kuhakikisha tunaendelea kuimarisha na kuzingatia mifumo ya ndani ya usimamizi na matumzi ya fedha za Umma" amesema Gamba.
Amesema ni muhimu kwa wakuu wa Idara, vitengo na sehemu kuhakikisha watendaji walio chini yao wanafahamu michakato yote ya matumizi ya fedha katika eneo lao sambamba na kujengewa uwezo wa kuzingatia kanuni na miongozo ya matumizi ya fedha za Umma.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa