Muonekano wamojawapo ya eneo la linaloelezwa kuwa awali ilikuwa ni makazi ya watu na zilipofanyika shughuli mbalimbali za kibiashara, mara baada ya mafuriko hayo katika mlima Hanang yaliyoambatana na tope zito pamoja na mawe kuharibu kabisa eneo hilo.
Muonekano wa Mlima Hanang unaotajwa kuwa ndio chanzo cha mafuriko hayo ukionekana kwa mbali nyuma ya makazi ya watu.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye alipotembelea moja wapo ya eneo lililoathiriwa na Mafuriko
Mnamo Desemba 3, 2023 wakazi wa kata ya Katesh wilayani Hanang Mkoani Manyara walikabiliwa na janga lililosababishwa na mvua kali iliyopelekea maporomoko makubwa yam awe na matope na kusababisha vifo ambavyo mpaka sasa mamlaka husika zimethibitisha kuwa vimefikia tisini na kusababisha majeruhi 139 huku idadi ya waathirika ikifikia 1,292.
Serikali ilijielekeza katika eneo hilo kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Hanang kukabiliana na adha mbalimbali ikiwemo kuimarisha ulinzi, kuondoa matope yaliyokuwa yamesababisha eneo hilo kutofanyika kwa kazi mbalimbali na kutopitika kabisa ili kuwafikia waathiriwa wa janga hilo na kuruhusu upatikanaji wa huduma za kijamii.
Serikali ilianzisha kambi maalum kwa ajili ya kuwahifadhi waliopata athari kubwa kutokana na janga hilo hususani waliopoteza makazi yao na kujikuta wakikosa huduma za msingi kama chakula, huduma za Afya, Maji na hata fedha ili kumudu kuendesha maisha yao ya kila siku.
Hizi ni hatua muhimu zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo ambalo limewaacha wenzetu wakazi wa Manyara wakipoteza ndugu, mali pamoja na makazi hali inayosababisha kukosa utulivu n ahata kutetereka kiuchumi.
Kwa kuguswa na uzito wa suala hilo, Uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi za kiserikali, binafsi, zile za kidini pamoja na watu binafsi walichangia vitu mbalimbali ikiwemo vyakula, vifaa mbalimbali pamoja na fedha Taslimu ambapo kwa ujumla wake vikifikia Thamani ya zaidi ya Shilingi Mil. 27.
Misaada hiyo iliwasilishwa wilayani Hanang na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Janeth Mayanja kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Akikabidhi misaada hiyo kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Mkoa Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimaoto na Uokoaji Thobias Andengenye alisema lengo la serikali mkoani mwake ni kuwagusa wanahanang kupitia misaada hiyo pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu katika kuwahudumia wananchi nyakati zote.
Aidha kupitia salamu za Mkoa kwa wakazi wa eneo hilo, Kiongozi huyo alisema sambamba na misaada hiyo, yeye binafsi aliguswa na tukio hilo na kuona ni vizuri kufika na kutoa pole kwa watendaji wa serikali pamoja na wananchi kwa kupoteza ndugu na mali zao.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mkuu wa WIlaya ya Hanag Janeth Mayanja alisema Serikali inaendelea kutoa huduma mbalimbamili kwa waathirika wa janga hilo ikiwemo kuwapatia matibabu, chakula, malazi huku mchakato unaoendelea ikiwa ni kuwapatia viwanja 269 vya makazi katika eneo jipya lililoandaliwa na serikali.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kwa kutambua kuwa moja wapo wa sekta iliyoathirika ni Elimu, Serikali imedhamiria kuhakikisha inakabiliana na changamoto hiyo kwa kuhakikisha wanafunzi walioguswa na maafa hayo wanapata sare mpya za shule, mabegi, daftari na kalamu kuendana na mahitaji yao.
Aidha mkuu huyo wa wilaya alimueleza mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuwa, serikali wilayani humo inaendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za jamii, kugawa mbegu kwa wakulima walioathiriwa na mafuriko hayo pamoja na kusimamia hali ya utulivu, Amani na usalama wa wakazi katika kipindi hiki ambacho wengi wao wamejikuta wakiwa katika hali ya kutoamini kilichotokea.
Pia Mayanja alitumia fursa hiyo kuwashukuru wanakigoma na watanzania kwa ujumla kwa moyo wao wa utu na uzalendo waliounesha na kuguswa kisha kujitoa kwa hali na mali ili kuhakikisha wanawarejeshea fuuraha wakazi wa Hanang.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa