Serikali Mkoani Kigoma imejipanga kuongeza ufanisi katika kuinua kiwango cha utekelezaji wa Afua za Lishe kufuatia Mkoa kushika nafasi ya 22 kitaifa kati ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara kwa mujibu wa takwimu zilizotokana na Tathmini ya Afua za Lishe Kitaifa kwa kipindi cha Mwaka 2021/2022.
Mkakati huo wa Pamoja umewekwa kwenye Kikao cha kusaini Mkataba Tendaji wa Lishe ngazi ya Jamii baina ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Wakuu wa Wilaya, pamoja na wakurugenzi wa Halmashauri mkoani hapa, kikiwa na lengo la kufanikisha suala la kuboresha hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika jamii pamoja na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mpango huo kwa ngazi ya Halmashauri.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika katika Halashauri ya Mji wa Kasulu, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alisema, kigezo kilichosababisha mkoa kushika nafasi hiyo ni kiashiria cha utoaji Fedha ambapo kwa kipindi cha Mwaka 2021/2022 kilitolewa kiasi cha Shilingi 630 badala ya Shilingi 1000 kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya Miaka mitano na kusababisha Mkoa kutoa Asilimia 80 ya Fedha ya Afua za Lishe.
‘’Kila halmashauri inajukumu la kutenga kiasi cha Shilingi 1000 kwa kila mtoto chini ya miaka mitano kwa lengo la kupunguza udumavu na kuimarisha afya zao kupitia upatikanaji wa lishe bora katika maeneo ya mkoa wetu, aidha kutokufanya hivyo ni kuwanyima watoto hao haki yao ya kimakuzi’’ alisema.
Alisistiza kuwa, halmashauri zote zihakikishe Fedha iliyotengwa kwa ajili ya Afua za Lishe kwa kipindi cha 2022/2023 inalingana na idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na iwapo bajeti iliyopangwa ni pungufu, marekebisho yafanyike haraka ili changamoto hiyo isijirudie.
‘‘Halashauri zihakikishe fedha iliyotengwa inatolewa yote na isitumike kwa kutekeleza shughuli nyingine tofauti na Afua za Lishe’’ alisema Andengenye.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kibondo Kanali Agrey Magwaza, alisema kwa kushirkiana na wakurugenzi wa Halashauri, wamekubaliana kuhakikisha kila robo itolewe Shilingi 250 ili ifikapo mwisho wa Mwaka ipatikane Shilingi 1000 kwa lengo la kufikia kigezo cha Utoaji fedha kama kilivyowekwa na Serikali.
Aidha, amewataka maafisa Lishe wawe wanatoa taarifa ya maendeleo ya ukusanyaji na uwasilishaji wa Fedha hiyo kwa wakuu wa wilaya ili kuwarahisishia ufuatiliaji wa fedha hiyo ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kushauri namna ya kuzitatua.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa viashiria na utatuzi wa Afua za Lishe, Afisa Lishe Mkoa wa Kigoma Naomi Lumenyela, alisema wakurugenzi wanapaswa kutoa fedha kuendana na Muongozo wa Serikali huku akisisitiza wazazi kuzingatia miongozo ya ulishaji wa chakula kwa watoto pamoja na utoaji wa Elimu ya Lishe kwa Jamii ili kupunguza tatizo la utapiamlo na udumavu.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255738192977
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa