Kazi nzuri zinazotekelezwa katika utoaji Msaada wa kisheria Mkoani Kigoma zimeendelea kuzaa matunda na kupunguza machungu katika jamii kutokana na uwepo wa changamoto ya uelewa duni kuhusu masuala ya kisheria hali inayosababisha upotevu wa mali, muda, uwepo wa chuki na uvunjifu wa amani na badala yake kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wahitaji wa msaada huo.
Msaada wa kisheria ni huduma inayojumuisha utoaji wa ushauri wa kisheria, usaidizi na uwakilishi wa watu wasiokuwa na uwezo kumudu gharama za uendeshaji wa kesi katika ngazi mbalimbali za kimahakama nchini.
Sheria inayoongoza utoaji wa Huduma ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya Mwaka 2017, imelenga kuwafikia wananchi walioko katika Mazingira yanayofikika na yale yasiyofikika isipokuwa kwa Kibali maalum ili kutoa msaada, ushauri, uwakilishi kwa watu hao kutokana na kukosa uwezo wa kumudu gharama za uendeshaji wa kesi au uelewa mzuri kuhusu haki zao kisheria.
Serikali katika Mkoa wa Kigoma imeendelea kutekeleza zoezi hilo kwa ufanisi na mafanikio makubwa pamoja na uwepo wa uhaba wa vitendea kazi na watendaji, huku ikama ikibainisha uwepo wa wasaidizi wa kisheria 117, watoa huduma ya msaada wa kisheria 10 na mawakili 12 ambao wanafanya kazi kwa ukaribu na kuendelea kuwajengea uwezo wasaidizi wa kisheria.
Msajili Msaidizi wa watoa Huduma za Msaada wa Kisheria Ngazi ya Mkoa Msafiri Nzunuri, anasema awali changamoto ya uelewa wa Masuala ya kisheria kwa wananchi ilikuwa kubwa, hali iliyosababisha mrundikano wa kesi Mahakamani na ongezeko la malalamiko kuhusu masuala ya upatikanaji wa Haki katika Jamii.
Anaeleza kuwa, kupitia mazoezi mbalimbali ya hamasa, uelimishaji pamoja na uhabarishaji kwa Umma kwa kutumia vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii, wameweza kuwafikia wananchi na kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu huduma za msaada wakisheria.
Anabainisha kuwa, idadi ya waliopata Msaada huo kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021 huduma za kisheria zilitolewa zilifanikiwa kuwafikia watu 526, huku rufaa zikiwa 81 na kesi zilizofanikiwa kufikishwa mahakamani zikiwa 15.
Msafiri anabainisha kuwa, kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022, idadi ya waliopata msaada wa kisheria kimkoa ni watu 917 ambapo kati yao ni Wanaume 136 na Wanawake 777 ikiwa ni ongezeko la watu 251.
Aidha anaongeza kuwa katika kipindi cha Julai 2021 hadi 2022, Msaada wa kisheria umefanikiwa kuwagusa watoto 913 ambapo kati yao wakiume wakiwa 136 na wakike 777 na kuhakikisha watoto hao haki zao zimepatikana kisheria.
‘‘Watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa kutosimamiwa ipasavyo kwa Sheria katia jamii na inapaswa kulichukulia suala hili kwa uzito vinginevyo tutajenga Taifa lenye watu wenye chuki na visasi kutokana na maumivu waliyowahi kuyapitia’’anasema Nzunuri.
Nzunuli anabainisha kuwa, changamoto zinazokwamisha kufikiwa kwa ufanisi ni utendaji usiozingatia kanuni wa Mabaraza ya Ardhi ya Kata, hususani katika kutafuta suluhu za migogoro ya Ardhi katika maeneo mbalimbali ya vijiji.
Anafafanua kuwa, baadhi ya watendaji katika Mabaraza hayo, wamekuwa wakijipa majukumu ya kuhukumu badala ya kutoa suluhu hali inayoendelea kusababisha wananchi kutoridhika na maamuzi yanayotolewa na kuamua kujielekeza katika ngazi mbalimbali za kimahakama ili kutafuta ufumbuzi wa kisheria wa masuala yao.
Anasema uelewa mdogo wa Jamii kuhusu Sheria unaendelea kusababisha changamoto kubwa katika utekelezaji wa mipango kazi iliyowekwa na Serikali ili kutekeleza jukumu hilo lenye dhamira ya kutoa haki kwa wanaoshindwa kuipata kutokana na sababu za kiuchumi na uelewa wa kisheria.
Ili kukabiliana na changamoto hizo Nzunuri anasema, wameendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya kisheria katika kuwajengea uelewa wananchi kwa kuendesha mafunzo mbalimbali pamoja na kutoa Elimu kwa mabaraza ya kata mkoani hapa.
‘‘Vyombo vya Habari pamoja na wadau kutoka Taasisi zisizo za kiserikali za HEKA, KIPAFO, WAPAO, BUPAO, MAPAO, KIPACE, BAKAIDS, KIVULINI, TWCC, KIVIDEA, WPC, KIWODE, KIWOHEDE, TGNP na WLAC wameendelea kuwa msaada katika kutoa elimu na kufanikisha utekelezaji wa kazi mbalimbali zinazohusu utoaji wa Misaada ya kisheria kwa jamii katika Mkoa’’anasema.
Katika kuhakikisha huduma za kisheria zinaendelea kutolewa katika wigo mpana na utoshelevu, Nzunuri anasisitiza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sheria wataendelea kuhakikisha utoaji bora wa huduma kwa kuwajengea uwezo wasaidizi wa Sheria katika Halmashauri zote, kuendeleza ushirikiano wa karibu na mawakili, kuongeza idadi ya walengwa pamoja na kuzidi kutoa Elimu kwa Jamii.
Huduma za kisheria zimeendelea kuwa msaada mkubwa mkoani Kigoma na Tanzania kwa ujumla kutokana na kuwafikia wahitaji katika maeneo fikika na yasiyofikika ila kwa kibali Maalum ambako mahitaji ni makubwa.
Aidha, Huduma za Msaada wa kisheria zimekuwa zikiwanufaisha kwa kiasi kikubwa wanawake, wazee, watoto na watu wenye mahitaji maalum ambapo baadhi ya wanajamii wasioheshimu sheria , haki za binaadamu, utu na mahusiano mema wamekuwa wakidhulumu kwa makusudi au kwa kutokuelewa haki za Raia za kisheria za makundi hayo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa